Kada wa CCM, Joseph Butiku ambaye amewahi kuwa msaidizi wa Rais wa Awamu ya Kwanza Mwalimu Julius Nyerere amesema tabia iliyoibuka ya watu kuhamahama vyama vya siasa inasababishwa na wanachama wanaokosa msimamo.
Butiku alitoa kauli hiyo baada ya kuulizwa maoni yake kuhusiana na wimbi la wanasiasa, wabunge na madiwani kuachia nyadhifa zao na kuhamia kwingine huku wakitoa lawama na tuhuma katika vyama wanavyovihama na kutoa sifa kule wanakohamia.
Vyama vilivyokumbwa na hamahama ya viongozi wake kwa siku za karibuni ni ACT Wazalendo, Chadema na CCM ambacho kinaonekana kuvuna zaidi kutoka katika vyama hivyo viwili.
Butiku alisema kuhama hata kama ni makazi inaruhusiwa kulingana na roho ya mtu inavyopenda, lakini wakati mwingine kitendo hicho kinaonyesha ni dalili ya kukosa msimamo.
“Watu wanatoka katika chama chenye msimamo wanasema msimamo hapo haupo wanakwenda huko. Wakati mwingine wanatoa matusi mengi na kashfa ya huko wanakotoka. Wakifika wanasema huku ndio tumefika kubaya kabisa, wanarudi wanasema huku tulikotoka kumbe pazuri. Mimi nina shaka sana na watu wa namna hii lazima niseme,” alisema Butiku.
“Sasa walikotoka wanasema pananuka baada ya muda wanasema kule ndio pananuka zaidi, wanarudi wanasema huku sasa afadhali. Wako wanaosema mzee (John) Magufuli sasa anasafisha CCM tunayoitaka, lakini wengine sikuwahi kuwasikia wakisema yale mabaya ya CCM kabla ya Magufuli kuingia madarakani.”
Butiku, ambaye alikuwa msaidizi wa Mwalimu Nyerere tangu akiwa madarakani na hata baada ya kustaafu alisema hana hakika kama hao wanaorudi CCM wamejitathmini na wanakubaliana na misingi na misimamo waliyoikimbia awali.
Alisema itikadi ya CCM ni ujamaa na kujitegemea na ipo kwenye Katiba ya nchi na katiba ya chama na kwamba ujamaa ni usawa na kuwatendea haki watu wote.
“Si kurudi tu CCM, lazima ukubali CCM ina maana yake, kwamba haina dhuluma, haina ubinafsi, haina wizi, haina ulaghai, inataka ufanye kazi kwa bidii, haina tamaa, inapenda watu, iko tayari kuwatumikia, hiyo ndiyo CCM. Ukirudi hapo uko tayari kwa yote hayo au unarudi kwa sababu umekosa nafasi kule, unarudi ambako unaweza ukaipata? Mimi nauliza maswali tu,” alisema Butiku na kuongeza hicho walichokimbia awali huku wanakorudi kimebadilika?
Watumishi wa umma na siasa
Akijibu swali kuhusu hali iliyojitokeza sasa ya baadhi ya watumishi wa umma hasa walio kwenye nafasi za maamuzi kutangaza hadharani kujiunga na chama cha siasa, alisema wakati wa mfumo wa chama kimoja lilikuwapo, lakini utaratibu huo uliondolewa wakati wa mfumo wa vyama vingi.
“Katibu mkuu (wa wizara serikalini) haruhusiwi kuwa mwanachama wa chama fulani wala kwenda kwenye mikutano ya chama hicho na wala kuonyesha unashabikia chama hicho, zipo ngazi za viongozi ambao hawaruhusiwi kushabikia vyama vya siasa, nadhani hata wakurugenzi. Mwishowe utageuza wizara yako tawi la chama,” alisema Butiku ambaye ni mwanachama wa CCM.
Alisema kwa watumishi wa umma hasa walio kwenye ngazi za maamuzi kama kuna vyama vya siasa wanavipenda hiyo inakuwa ni siri yao ambao huitumia wakati wa kupiga kura.
Hata hivyo, Butiku alisema watumishi wa ngazi za chini ambao hawana mamlaka yanayoweza kuathiri utendaji wao kwa ushabiki wa kisiasa, hao wanaweza kushabikia vyama. “Ingawaje mimi nafikiri chama ni chama; na serikali ni serikali,” alisema.
“Mimi nafikiri tungekuwa na uamuzi wa uhakika ukiwa mtumishi wa Serikali hauwezi kuingia kwenye chama chochote. Ukitaka kuingia kwenye chama nenda kwenye chama kwa sababu ni vigumu sana kutenganisha mambo haya, imani ya chama na mahitaji ya sheria na Katiba.
“Unaweza ukasema (mtu fulani) asipewe kazi kwa sababu yeye ni wa chama fulani.
“Iko mifano mingi tu, hapa Bara huko Zanzibar. Watu wanazungumza ‘sisi hatupati kazi kwa sababu ni wa CCM au wa CUF’ inategemea nani yuko serikalini na inakwenda hadi chini.”
Siasa vyuoni
Akifafanua hoja yake, Butiku alizungumzia suala la siasa kuingizwa vyuoni kuwa umeharibu utamaduni wa kujenga hoja kisomi.
“Mfano, nchi yetu imetumbukiza siasa katika vyuo vikuu, mimi naamini wametuharibia vyuo vikuu. Pale ni sehemu ya kutafuta ukweli. Sasa mkianza kubishana katika kutafuta ukweli mmoja anachomoka wewe Chadema, wewe CCM, wewe nilijua ni CUF,” alisema.
Butiku alisema kitendo cha kuingiza siasa kwenye vyuo vikuu kimeua mfumo wa hoja na hatari yake wasomi watakaotoka pale watakuwa ni wenye imani ya vyama vya siasa badala ya kuwa na imani ya nchi yao.
“Tukianza kupata maprofesa waliogawanyika kwa itikadi za vyama na ushabiki ni hatari katika maendeleo yetu. Nani anataka ushabiki katika vyuo vikuu, alihoji Butiku.
Mikutano ya vyama vya siasa
Butiku alizungumzia kuzuiwa kwa mikutano ya siasa akisema anaungana na Rais John Magufuli kwa sababu wananchi wanataka maendeleo siyo mikutano na maandamano ya kisiasa yasiyokwisha.
“Mimi ninakubaliana na Rais (John) Magufuli hizi siasa za njooni, njooni, kila asubuhi wanachama njooni, njooni, kesho wanachama njooni, njooni, kesho wazee njooni, njooni. Mimi nadhani haina maana sana, ni demokrasia, lakini ni aina ya demokrasia hewa. Haimpi chochote cha maana yule anayekusanyika kwenye mikusanyiko hiyo,” alisema Butiku.
Alisema baada ya uchaguzi kuna utamaduni wa vyama vya siasa hasa vya upinzani kufanya mikutano ya hadhara maeneo mbalimbali mikoani wakidai kuibiwa kura, hasa pale wanapokuwa wameshindwa kwenye uchaguzi.
Butiku alisema vyama vya siasa vilivyoshindwa kwenye uchaguzi vinatakiwa kwenda mahakamani na si kulalamika kwenye mikutano ya hadhara, tena wakiwa wametoa hukumu kwamba wao ndio washindi.
“Rais amesema vizuri maendeleo ni wananchi, wananchi wetu katika mambo ya kisiasa wako katika majimbo, huko tuwe huru kusema chochote kwa sababu kule tuko karibu na wananchi na tunazungumza nao kuhusu mambo yao,” alisema Butiku.
chanzo:Mwananchi.
Comments