Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya amesema kuwa umoja huo unaunga mkono makubaliano yaliyofikiwa kati ya Bangladesh na Myanmar ya kurejea nyumbani wakimbizi wa Kiislamu wa jamii ya Rohingya.
Federica Mogherini amesema kuwa, kutiwa saini kati ya nchi hizo makubaliano kuhusiana na kurejea nchini kwao wakimbizi Waislamu wa jamii ya Rohingya ni hatua muhimu katika jitihada za kuupatia ufumbuzi mgogoro huo.
Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya ameyataja makubaliano hayo kwamba ni hatua moja mbele ya kuupatia ufumbuzi moja ya migogoro mibaya kabisa ya kibinadamu katika zama hizi.
Federica Mogherini ameeleza kuwa, Umoja wa Ulaya utasimamia utekelezwaji wa makubaliano hayo na kuhakikisha kwamba, kurejea makwao wakimbizi Waislamu wa jamii ya Rohingya kunaendana na sheria za kimataifa.
Hayo yanajiri wakati mashirika ya kimataifa yasiyo ya kiserikali yakisema kuwa, hatua za serikali ya Myanmar dhidi ya Waislamu wa Rohingya ni jinai za wazi dhidi ya binaadamu ambapo sambamba na kulaani jinai hizo yameitaka dunia kukabiliana na serikali ya nchi hiyo ili kuzuia hali hiyo.
Maelfu ya Waislamu wa kabila la Rohingya nchini Myanmar wameuawa na maelfu ya wengine kujeruhiwa tangu kuanza wimbi jipya la mashambulizi ya jeshi na Mabudha wenye misimamo mikali katika mkoa wa Rakhine magharibi mwa nchi nchi hiyo tangu tarehe 25 Agosti mwaka huu hadi sasa.
chanzo:parstoday.
Comments