Mke wa mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu, amesema angependa kuwajua watu waliomshambulia mumewe, aliyewaamuru wafanye shambulio hilo na sababu za kufanya uovu huo.
Mke huyo ambaye pia ni wakili, Alicia Magabe anasema kuwafahamu watu hao ni muhimu kwa kuwa familia haijui kwa sasa watu hao wanatafakari na kupanga kitu gani baada ya jaribio la kwanza la kumuua kushindikana.
Lissu, mmoja wa wanasiasa wasio na hofu kusema lolote wanaloliamini, alishambuliwa na watu wasiojulikana Septemba 7 akiwa ndani ya gari lililokuwa limewasili kwenye makazi yake Area D mjini Dodoma akitokea bungeni.
Tangu wakati huo, wakili huyo wa kujitegemea na mwanasheria mkuu wa Chadema, amelazwa Hospitali ya Nairobi nchini Kenya na hadi sasa Jeshi la Polisi halijaeleza kama limeshapata fununu ya waliohusika zaidi ya kujibu kuwa linaendelea na upelelezi kila waandishi wanapotaka kujua maendeleo ya suala hilo.
Na sasa mke huyo wa Lissu na ambaye pia ni wakili, Alicia Magabe anataka kuwajua waliomfyatulia mumewe zaidi ya risasi 30, aliyewatuma na sababu za kuwatuma.
Magabe pia anasema familia yake kwa sasa ipo shakani kwa kuwa hajui hao waliofanya shambulio hilo ambalo linaonekana la kukusudia kumuua, wanatafakari nini na kupanga nini.
Akizungumza na Mwananchi katika Hospitali ya Nairobi, Wakili Magabe alisema Lissu ametumia sehemu kubwa ya ujana wake kupigania masilahi na haki za Watanzania, hivyo angependa kuona haki inatendeka.
“Binafsi nimewasamehe kwa kitu walichokifanya, lakini hiyo haina maana kwamba nisingependa kuona haki inatendeka,” alisema wakili huyo.
“Sitaki kuwe na mkanganyiko baina ya kusamehe na hali ya kutamani kuona haki inatendeka.”
Alisema
tukio hilo limemfanya aanze kuamini kuwa kuna watu walitaka kumuua
Lissu, lakini hawajafanikiwa na anaamini watu hao wapo, hivyo anahofia
usalama wa familia yake.
“Mpaka sasa sijasikia kama kuna uchunguzi wowote umefanyika na sijawahi kusikia watu wamekamatwa,” alisema Wakili Magabe.
“Hivyo
nawaza kuwa hayupo salama na mimi kama mke wake sijisikii kama niko
salama sana. Nawaza hawa watu watakuwa wanatafakari au wanapanga nini.
Hiyo ndiyo hali niliyonayo kwa sasa. Sijui hao watu wako wapi.”
Hata
hivyo, Wakili Magabe alisema Lissu yuko imara na shambulio hilo
halijamrudisha nyuma katika harakati zake za kupigania haki na za
kisiasa.
Alisema hilo alilionyesha mara tu alipopata fahamu.
“I
have survived to tell a tale, I have lived to tell a tale (nimeepuka
kifo ili nieleze jambo) ndivyo alivyosema baada ya kuzinduka,” alisema
Wakili Magabe.
Alisema baada ya fahamu kumrejea sawasawa amekuwa akizungumza maneno yanayoashiria kwamba ana ari zaidi.
“Spirit
yake ipo very high (ari yake iko juu sana). Si mtu wa kusema kuwa baada
ya tukio amekuwa mnyonge, mwoga au ujasiri wake umepungua,” alisema
wakili huyo.
“Sijawahi
kupata hata kauli yake moja inayoashiria kwamba sasa atarudi nyuma.
Kama mke nataka mume wangu apone, tutoke hospitali turudi nyumbani.
Lakini wanapokuja viongozi wenzake kutoka Tanzania; wastaafu na wa sasa
na hata hapa Kenya, kauli zake zote zinaashiria amekua zaidi kisiasa.
“Anasema ‘kuna siku nitapona na nitaendelea na kazi zangu’ ili kuwatia moyo wanasiasa na wanaharakati.”
Kuhusu mumewe kuendelea na siasa baada ya kupona, Wakili Magabe alisema Lissu ndiye anaweza kulizungumzia suala hilo.
“Mimi
nikiwa msaidizi wake wa kwanza, nitakuwa mtu wa mwisho kusema Lissu
asifanye analotaka kwa kuwa hata akiyatamka hayatakuwa na nguvu mbele za
Mungu,” alisema.
“Binafsi
nasema alikuja duniani kwa makusudi. Mungu alimleta duniani kwa sababu
na alijua hata kabla hajazaliwa maisha yake yatakuwaje na atafanya nini
hapa duniani.
“Sidhani
kama kuna binadamu anaweza kuzuia yale ambayo Mungu amepanga. Sitaki
kusema kama ataendelea na siasa, hataendelea nazo, yupo kwa kusudi
lake.”
Magabe
alisema kuna watu wanapigwa risasi moja na wanafariki dunia, lakini
Lissu alipigwa risasi 16 za moto ambazo zilipita kwenye mwili wake na
anaendelea kuishi.
Alisema
anafarijika kuona Lissu yu mzima kwa kutumia nguvu za watu wote ambao
kwa namna moja au nyingine wanapenda aishi, akianzia na waliochanga
fedha, waliomtolea damu, walioomba, waliomnyanyua, waliomtibu mara ya
kwanza na wanaoendelea kumtibu.
“Hatujawahi
kuwa peke yetu na nimegundua kumbe kupigwa risasi kwa Lissu ni tukio
ambalo limewagusa Watanzania na mataifa mengi na wapo tayari kusaidia,”
alisema mwanamke huyo.
“Hii ni kwa kuwa ametumia ujana wake kupigania masilahi na haki za Watanzania.”
Magabe
alisema risasi zilizompata Lissu ziliharibu zaidi mifupa, tishu zilizo
karibu na mifupa ya mguu wa kulia na mikono, lakini hakuumia kwenye
neva, mishipa mikubwa ya damu, ya fahamu au ogani.
“Madaktari wanasema risasi zilikuwa zinakwepa maeneo muhimu. Ni kitu ambacho hawajawahi kukiona,” alisema.
“Hapa
kuna mshipa mkubwa wa damu, lakini risasi imepita pembeni. Walikuwa
wanashangaa inawezekana vipi risasi nyingi zikaingia lakini zikakwepa
maeneo muhimu.”
Alisema
madaktari wamemweleza Lissu kuwa ataendelea kuimarika lakini itachukua
muda kabla hajapona na kuweza kutumia viungo vyake vyote kama kawaida.
Mama
huyo alisema awamu ya kwanza ilikuwa kumtibu majeraha na ya pili ni
kumjengea uwezo wa kutumia viungo vyake ili baadaye aweze kusimama na
kurudi katika hali yake.
Magabe
alisema ilichukua mwezi mmoja Lissu kutoka ICU na hakuweza kumhudumia
kwa ukaribu kutokana na masharti ya chumba cha uangalizi maalumu.
“Kila
siku naamka kama nakwenda kazini. Lazima niamke asubuhi kuja hospitali
kisha narudi usiku nyumbani. Siruhusiwi kulala hapa,” alisema.
Simulizi ya siku ya tukio
Magabe
alisema siku ya shambulio alikuwa ametoka Kerege wilayani Bagamoyo na
alipanga kukutana na rafiki yake eneo la Mpiji, Bunju.
“Saa
6:30 nilifika kwake, akaniambia lazima nipate chakula cha mchana, baada
ya chakula nilimwambia nipumzike kwenye kochi,” alisema.
“Baada ya dakika 25 akaniamsha akaniambia Alicia amka ukilala sana mchana huu usiku unaweza usipate usingizi,” alisema.
Alipoamka
aliwasha simu zake na kukuta ujumbe usemao, “hello sister, kuna taarifa
inazunguka sina hakika kama ni ya kweli. Kama kweli pole sana dada
yangu.”
Alisema
moja kwa moja wasiwasi ulimjia kwamba huenda mumewe amekutwa na jambo
baya, alisema alichowaza awali huenda amepata ajali na ndipo akamuomba
rafiki yake ampigie mtu huyo simu kujua zaidi kuhusu ujumbe huo.
“Niliingia
kwenye magroup ya Whatsapp ya Chadema nikakutana na hiyo taarifa.
Nilipiga kelele kwa nguvu, rafiki yangu aliniuliza umeona nini
nikamwambia kuna ujumbe huu,” anasema na kumpa rafiki huyo simu asome
ujumbe huo uliosema “Tundu Lissu amepigwa risasi.”
“Nilianza
kuwaza yupo hai au amekufa. Niliwaza nifanye nini nikamwambia nataka
kwenda nyumbani. Huko niliamini kuwa ningewaza kwa utulivu nini cha
kufanya.”
Anasema baadaye simu zilianza kuingia mfululizo na ndipo alipoamini kuwa habari hizo ni za kweli.
“Nilimpa jukumu hilo (la kupokea simu) kwa sababu ni rafiki yangu wa karibu tangu sijaolewa,” alisema.
Baadaye waliingia kwenye gari na yeye kuanza kuendesha huku rafikiye akizungumza na waliokuwa wakimpigia simu.
Magabe
alisema baada ya kuiingia mtaa wa nyumbani kwake, aliona vijana
wanamwangalia katika namna ambayo ilionyesha kuna kitu wanakijua.
“Mwonekano wao ulikuwa tofauti wananiangalia kwa huruma, kwa mshangao.
Wanatamani waongee,” alisema.
Anasema
nyumbani aliwakuta shemeji zake wawili na mtoto wa baba yake mdogo,
lakini alishindwa kuingia ndani na badala yake alikaa bustanini.
“Nilipigiwa
simu na watu waliokuwepo hospitali na wakaniambia ni kweli amepigwa
risasi, lakini yupo hai. Walinitaka nitulie mpaka nitakapopewa taarifa
nini cha kufanya,” alisema.
Alisema mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alimweleza nini cha kufanya kwa wakati huo.
Alisema
baadaye aliambiwa Lissu angepelekwa Nairobi na hivyo aende uwanja wa
ndege kwa ajili ya safari ya Dodoma na baadaye Nairobi.
Aliondoka na kaka yake na marafiki wa karibu, lakini alipigiwa simu na kutakiwa kushuka kwa kuwa muda haukuwa rafiki.
“Nilipanda bodaboda,” alisema.
“Wale
vijana walikimbiza sana na ilikuwa ni mara ya kwanza kupanda pikipiki
Dar es Salaam. Niliogopa na kusali Mungu anisaidie kufika uwanja wa
ndege salama.”
Alipofika Dodoma ndipo alipomuona kwa mara ya kwanza Lissu tangu apate taarifa za shambulio.
“Baada
ya dakika chache akaja akiwa kwenye kitanda kutoka chumba cha upasuaji.
Kwa kumuangalia nilijua ameumia sana hakuwa anajitambua,” alisema.
Comments