Utafiti: Rushwa imepungua nchini Tanzania

Utafiti: Rushwa imepungua nchini TanzaniaMatokeo ya utafiti wa Taasisi ya Twaweza yameonesha kuwa asilimia 85 ya wananchi wa Tanzania wanaripoti kuwa, viwango vya rushwa vimepungua katika nchi hiyo kwa mwaka 2017 ikilinganishwa na mwaka 2014 ambao asilimia 78 walisema viwango vya rushwa vilikuwa vikubwa kuliko miaka 10 iliyopita.


Aidha, utafiti huo umebainisha kwamba, wananchi wameripoti kuwa uzoefu wao wa kuombwa rushwa umepungua katika sekta zote mwaka huu ikilinganishwa na 2014. 

Akiwasilisha matokeo ya utafiti huo Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza, Aidan Eyakuze amesema matokeo hayo yametolewa kupitia utafiti unatokana na takwimu kutoka Sauti za Wananchi, utafiti wa kwanza barani Afrika wenye uwakilishi wa kitaifa unaotumia simu za mkononi.
Matokeo hayo yanatokana na takwimu zilizokusanywa kutoka kwa wahojiwa 1,705 kutoka maeneo mbalimbali Tanzania Bara kati ya Julai na Agosti mwaka huu,” alibainisha Eyakuze.
Ameongeza kuwa, matokeo hayo ya utafiti yanatia matumaini ikilinganishwa na miaka mitatu iliyopita, ambako wananchi wamekuwa na mtazamo chanya kuhusu mafanikio yanayojitokeza kutoka katika mapambano dhidi ya rushwa.
Mwakilishi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Sabina Seja amesema kwamba, rushwa bado ipo na kuwataka wananchi na wadau mbalimbali kutoa ushirikiano katika kupambana nayo badala ya kuiachia serikali pekee.
Naye Ludovick Utouh aliyekuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), amesema ni kweli kwa kipindi hiki rushwa imepungua tofauti na miaka ya nyuma na kuwataka Watanzania kuichukia rushwa.
Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza, Aidan Eyakuze, alisema wananchi wanaripoti kuombwa rushwa katika sekta mbalimbali kumepungua ambapo kwa upande wa polisi ilikuwa asilimia 60 mwaka 2014 hadi asilimia 39 mwaka 2017, Ardhi asilimia 32 mwaka 2014 hadi asilimia 18 mwaka huu, Afya asilimia 19 mwaka 2014 hadi asilimia 11 mwaka huu.
chanzo:parstoday.

Comments