Butiku: Katiba Z’bar inataka Umoja wa Kitaifa, isipuuzwe.

Joseph Butiku, ambaye alikuwa msaidizi wa Rais wa kwanza, Mwalimu Julius Nyerere amesema Katiba ya Zanzibar inaeleza kuwa na Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), hivyo haifai kupuuzwa kwa kuwa inalenga kusaidia yeyote yule na kupunguza makali ya ubinafsi.
“Katiba ya Zanzibar inasema mkitaka kubadili mnarudi kwa wananchi. Huwezi kusema haikusema hivyo,” alisema Butiku katika mahojiano maalumu na Mwananchi wiki hii.
“Na hili nalisema kama mzee, sina taasisi ya kulisemea. Nyerere amekufa anasema mnapuuza Katiba, huyo ni mzee ameanzisha Taifa hili anatoka anatuambia moja ya nyufa ni kwamba mnapuuza Katiba na mnapuuza sheria.”
Baada ya vurugu za mwaka 2001 zilizotokana na Uchaguzi Mkuu na baadaye mwaka 2005, CCM na chama kikuu cha upinzani cha CUF waliingia katika mazungumzo yaliyoishia kukubaliana kubadili katiba na kuanzisha Serikali ya Moja wa Kitaifa.
Serikali hiyo ilifanya kazi kwa kipindi kimoja tu (2010 hadi 2015). Uchaguzi wa mwaka 2015 uliingia dosari na baadaye CUF kukataa kushiriki katika uchaguzi wa marudio na hivyo CCM kukosa mshirika wa kuunda naye SUK kwa mujibu wa katiba.
Mshindi wa uchaguzi huo, Dk Ali Mohamed Shein ameunda serikali yake bila ya makamu wa kwanza wa rais anayetajwa katika katiba na Butiku anaona Baba wa Taifa alishaona mbele.
“Nadhani alinusa. Hilo limetokea yupo na sisi limetokea (wakati) tupo. Haifai kupuuza Katiba wala haifai kuivunja sheria. Katiba ipo ili kusaidia yeyote yule katika ngazi yeyote kupunguza makali ya ubinafsi,” alisema.
“Ukitoka hapo unagota, Katiba inasema hii hapana. Inakuwa kama kaa la moto.
“Katiba lazima iwe kaa la moto. Ikisema ili kubadili lazima muende kwa wananchi, inabidi muende kwa wananchi. Kwa sababu msipokwenda mnaacha nafasi, nyinyi mtafurahi, (lakini) mnaacha nafasi ya ubishi kwa sababu miiko mliyokubaliana mmevunja.
“Na mwiko ukivunjwa huwa na madhara yake. Madhara yake huwa hayaishi, kama ni maisha ya Kiafrika mpaka mtambike.”
SUK imetamkwa katika Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 Toleo la 2010 Kifungu cha 9(3). Kifungu hicho kinasema “muundo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar utakuwa wa Umoja wa Kitaifa na utendaji wa kazi zake, utafanywa katika utaratibu utakaohakikisha kuendelezwa kwa umoja nchini na lengo la kufikia demokrasia”.
Katiba hiyo ilianzisha cheo cha makamu wa kwanza wa Rais na makamu wa pili na kufuta wadhifa wa Waziri Kiongozi.
Kwa mujibu wa Marekebisho ya 10 ya Katiba, makamu wa kwanza wa Rais atateuliwa na Rais baada ya kushauriana na chama cha siasa kilichopata nafasi ya pili katika matokeo ya kura ya uchaguzi wa Rais.
Kifungu cha 39(3) cha Katiba hiyo kinasema makamu wa kwanza wa Rais atatakiwa awe na sifa za kumwezesha kuchaguliwa kuwa mjumbe wa Baraza la Wawakilishi na atateuliwa na Rais baada ya kushauriana na chama kilichopata nafasi ya pili katika matokeo ya kura ya uchaguzi wa Rais, kama chama hicho kilichopata nafasi ya pili katika matokeo ya kura ya uchaguzi wa Rais, kitapata asilimia kumi ya kura zote za uchaguzi wa rais.
Katiba hiyo inasema makamu wa pili wa Rais atateuliwa na Rais kutoka miongoni mwa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kutoka katika chama cha siasa anachotoka Rais.
Hata hivyo, hii si mara ya kwanza kwa Zanzibar kuingia katika shutuma kama hizo.
Mwaka 1993 wakati wa utawala wa Serikali ya awamu ya pili chini ya Rais Ali Hassan Mwinyi, Zanzibar ikiwa inaongozwa na Dk Salmin Amour ilijiunga na Jumuiya ya Umoja wa Nchi za Kiislam (OIC), kitendo kilichoelezwa ni kuvunja Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mwalimu Nyerere alisema kitendo hicho ni kuvunja Katiba na ndani ya Bunge kuliibuka kundi la wabunge 55, wakiongozwa na aliyekuwa mbunge wa Chunya (CCM), Njelu Kasaka walioanzisha hoja kutaka Serikali ya Tanganyika ndani ya Muungano kutokana na sakata hilo la OIC. Hata hivyo, hoja hiyo ilizimwa na Zanzibar kulazimika kujitoa OIC.
Kulingana na Butiku, Nyerere alishuhudia uvunjaji huo wa Katiba lakini kauli yake kwamba “na sisi limetokea tupo” ni kuhusu kutoundwa kwa SUK.
Dk Shein na Maalim Seif
Butiku pia aliwazungumzia mahasimu wa kisiasa, Dk Shein na Maalim Seif Sharif Hamad, akisema kama ikitokea akakutana nao atawaambia wasisahau kuwa wao ni Watanzania na wamepewa jukumu la kuongoza Wazanzibari.
Alisema jukumu lao ni kuwaletea Wazanzibari maendeleo katika hali ya amani na utulivu. “Sidhani kama wana tofauti kubwa kuhusu maendeleo ya Wazanzibari,” alisema.
“Maana Wazanzibari wanataka elimu, wanataka afya, wanataka barabara, wanataka amani, wanataka kusomesha watoto wao, wanataka nchi yao ijengwe vizuri, wanataka maji sidhani kama katika hayo wanatofautiana.”
Butiku alisema tofauti kati ya viongozi hao ni nani atawale, badala ya kufuata utaratibu unaotoa fursa kwa wananchi kuamua kiongozi gani wa kuwatawala.
“Nasema kama mzee tu, chaguzi mara nyingi zinaleta ubishi kwa sababu viongozi wanabishania ushindi, lakini ushindi huwa umekwishatolewa na wananchi,” alisema.
“Tatizo linatokea huwa viongozi hawatuambii ukweli wananchi wameamua nini.”
chanzo:Mwananchi.

Comments