
Alisema mradi wa TASAF ulioongeza chachu ya uzalishaji kwa Wananchi hao
kutokana na kuanzishwa kwa miradi mingi ya uzalishaji utaendelea
kuongezewa nguvu na Benki ya Dunia katika azma ya kuikomboa Jamii ya
Watu wa kipato cha chini.
Bwana Michal Rutkowski alitoa kauli hiyo wakati wa mazungumzo yake na
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Vuga Mjini
Zanzibar akiuongoza Ujumbe wa Viongozi wa Benki ya Dunia uliopo
Zanzibar kukagua Miradi inayosimamiwa na kufadhiliwa na Taasisi hiyo ya
Fedha ya Kimataifa kupitia Mfuko wa TASAF.
Alisema uwajibikaji wa Wananchi wa Zanzibar hasa katika Miradi ya
Kiuchumi umeongeza ushawishi kwa Benki ya Dunia kufikiria kuongeza nguvu
zaidi za misaada ili kuona lengo lililokusudiwa la kuikomboa Jamii ya
wanyonge linafanikiwa vyema.
Mkurugenzi huyo ambae pia ni Mkuu wa Mtandao wa Masuala ya Kijamii
na Ajira wa Benki ya Dunia alizihakikishia Serikali zote mbili za
Tanzania kwamba Taasisi hiyo itaendelea kuongeza nguvu katika kuona
Miradi ya Wananchi wa kipato cha chini inaendelea kudumu kwa muda mrefu.

Mapema Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi
alisema mabadiliko ya Sera ya Ustawi wa Jamii katika kuwapatia posho
Wazee wa Zanzibar yamekuja kufuatia mchango mkubwa walioutoa Wazee hao
wakati wa utumishi wao kwa Taifa.
Balozi Seif alisema Wazee wengi hasa wale waliotumikia Taifa kupitia
Taasisi za Umma na hata zile Binafsi wana wajibu wa kuendelea kutunzwa
na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ili kuwapa faraja kutokana na
kazi yao kubwa waliyoifanya ya kujenga Taifa wakati wa Utumishi wao.
Akizungumzia Miradi ya Kijamii Balozi Seif alisema nia ya Serikali
Kuu katika kuwajengea uwezeshaji Kiuchumi Wananchi hasa wale walioko
katika mazingira magumu zaidi Vijijini umelenga kuwapunguzia ukali wa
maisha.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimuahidi Mkurugenzi huyo wa
Benki ya Dunia anayesimamia Mtandao wa Masuala ya Kijamii na Ajira
kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kushirikiana na
Taasisi hiyo katika kuona miradi iliyoanzishwa inafanikiwa vyema .
Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali
Iddi alikutana kwa mazungumzo na Uongozi wa Kamati Tendaji ya Taifa ya
Jumuiya ya Maulid ya Milad – Nabee Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Katika mazungumzo yao Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Maulidi
ya Mfuguo Sita Sheikh Sheral Chamsi alisema maandalizi ya Maulidi hayo
yanayotarajiwa kufanyika Alhamis ya Tarehe 30 Novemba Mwaka huu katika
Viwanja vya Maisara Suleiman yako katika hatua za mwisho za mafanikio.
Hata hivyo alisema endapo zitanyesha mvua siku hiyo ya Maulidi,
sherehe hizo zitahamishiwa katika Msikiti Mkuu wa Ijumaa wa Mushawar
uliopo Muembe Shauri Mjini Zanzibar.
Sheikh Sheral alisema matayarisho ya kuvipata vyuo vya Madrasa na
Wanafunzi watakaosoma kasida kwenye sherehe hiyo yameshakamilika baada
ya kufanya mchujo wa upatikanaji wake ulioshirikisha Wilaya zote za
Unguja na Pemba ambapo Mwaka huu umeibua Madrasa ya Jojo Pemba na
Tumbatu Gomani kwa upande wa Unguja.
Mwenyekiti huyo wa Kamati ya Maandalizi ya Maulidi ya Mfuguo Sita
alimueleza Balozi Seif kwamba maandalizi ya mwisho ya Maulidi hayo
yatafanyika baada ya sala ya Laasiri katika Msikiti Mkuu wa Ijumaa wa
Muembe Shauri.
Akitoa shukrani zake kwa Kamati hiyo, Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliupongeza Uongozi wa Kamati hiyo kwa
juhudi unazochukuwa wa kufanikisha maadhimisho ya Sherehe za Uzawa wa
Mtume Muhammad {SAW} ambazo ni muhimu katika kuendeleza Dini ya
Kiislamu.
Balozi Seif alisema Maulid yanaendelea kufanikiwa kila Mwaka na bado
haijatokezea kasoro yoyote ile jambo ambalo limeonyesha umahiri wa
Kamati hiyo katika utekelezaji wa Majukumu yake iliyopangiwa na Taifa.

chanzo: zanzibar24.
Comments