Novemba
22, mwaka 2016, Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe, aliweka picha yake
mtandaoni ikimwonyesha akiwa ndani ya Ikulu ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, akiwa miongoni mwa wageni walioalikwa kwenye tafrija ya rais
mpya wa nchi yetu, John Magufuli.
Katika
picha waliyopigwa inaonyesha dhahiri kuwa, kazi ya Rais mstaafu Jakaya
Kikwete ilikuwa kumtambulisha Zitto Kabwe kwa Rais Magufuli. Ni heshima.
Mara
kadhaa Zitto amesema picha hiyo inaonyesha ‘Rais wa 6” akiwa na marais
wa awamu ya nne (Kikwete) na tano (Magufuli). Ni ndoto ya kila
mwanasiasa kuwa kiongozi mkuu wa nchi. Lakini kuna sura tofauti kati ya
Zitto Kabwe wa serikali ya awamu ya nne na awamu ya tano ya John
Magufuli.
Katika
utawala wa Kikwete, Zitto amepitia katika matukio mbalimbali ya
kusisimua na kushangaza, huku mengine yakitawaliwa na utata machoni pa
wanasiasa wenzake. Hata hivyo, hizo si hoja za msingi kwa leo. Swali
kubwa la leo ni kwanini baadhi ya wanasiasa wa chama chake cha
ACT-Wazalendo wanamkimbia Zitto?
Si vibaya kuuelezea uzuri wa Zitto. Kwanza amejitahidi kufanya mbinu za kuwa hodari na kileleni.
Mwaka
2012 Zitto aliungana na wabunge kupaza sauti kutaka mawaziri nane
wang’oke kutokana na ufisadi. Zitto alikusanya saini za wabunge,
kutimiza 70, ili awasilishe hoja ya kumng’oa aliyekuwa Waziri Mkuu
Mizengo Pinda. Baadaye Rais Kikwete aliwang’oa mawaziri waliokuwa
wanatakiwa kuwajibishwa, hivyo akafanikiwa kumwokoa Pinda.
Mwaka
huo huo, Kamati ya POAC ilivunjwa na Spika wa Bunge la 10, Anne
Makinda, ambapo aliunganisha na Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC),
Zitto akashinda uenyekiti wake.
Aidha,
ni Zitto Kabwe ambaye alihakikisha anapigania masilahi ya Watanzania
baada ya kukubali kutimuliwa bungeni kutokana na tuhuma zake dhidi ya
aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi, ambaye alidaiwa
kusaini mkataba wa Buzwagi akiwa hotelini huko jijini London, nchini
Uingereza. Kutokana na tuhuma hizo, aliyekuwa Spika wa Bunge 2005-2010,
Samuel Sitta, alimfukuza bungeni.
Zitto pia amechangia pakubwa kupatikana kwa sheria ya Capital Gain kwenye sekta ya madini nchini.
Mapito ya Zitto
Zitto ni mwanasiasa aliyeibuliwa na Chadema chini ya uenyekiti wa Freeman Mbowe.
Ndicho
kipindi ambacho Zitto aliibuka kuwa mwanasiasa mahiri na aliyetikisa
kwa matukio mbalimbali. Tuhuma za usaliti wa Zitto dhidi ya Chadema
zilijiri zaidi wakati akiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali,
ambapo alimwagiza Msajili wa Vyama vya Siasa kufanya ukaguzi wa hesabu
zao za fedha.
Zitto
aliagiza hilo akiwa Naibu Katibu Mkuu Chadema, hali ambayo
ililalamikiwa kuwa anakisaliti chama, kwani alitakiwa “kuwatonya” juu ya
mpango huo wa ukaguzi. Wapo walioudhika juu ya mpango huo na kudai
Zitto ni msaliti.
Pili,
mwaka 2009 Zitto alitangaza bayana kumuunga mkono mgombea wa NCCR-
Mageuzi katika Jimbo la Kigoma Kusini, David Kafulila, licha ya chama
chake hicho cha zamani, Chadema kuweka mgombea wao.
Tatu,
uamuzi wa Zitto Kabwe kugombea uenyekiti mwaka 2009 dhidi ya Freeman
Mbowe lilikuwa jaribio ambalo Chadema kilitakiwa kukabiliana nalo na
kulitatua. Zitto akiwa na kambi yake ya kisiasa ndani ya Chadema,
alichukua fomu na kugombea uenyekiti, hali ambayo iliibua malumbano
makali, na kuitwa msaliti.
Kambi
ya Zitto Kabwe ilikuwa pamoja na Samson Mwigamba na Profesa Kitila
Mkumbo. Kwa muda mrefu Zitto alituhumiwa kutoshiriki majukumu mbalimbali
ya kichama, hali ambayo ilitokana na jaribio lake la kugombea
uenyekiti.
Inaelezwa
kuwa, Zitto hakuwa karibu tena na Chadema, ingawa mwaka 2010
aliruhusiwa kugombea ubunge wa Kigoma Kaskazini kwa tiketi ya chama
hicho. Kuutaka uenyekiti kulitajwa kama usaliti ndani ya Chadema.
Nne,
M4C ni moja ya operesheni inayotumiwa na Chadema ambayo Watanzania
wanahamasishwa kujiunga katika chama ili kuleta mabadiliko. Zitto
alidaiwa kutoshiriki kikamilifu katika operesheni hiyo.
Mwishowe
Zitto na Chadema wakapelekana mahakamani, licha ya katiba ya chama
kukataza wanachama wake kutokwenda mahakamani kwa suala la chama. Ndiyo
kusema Zitto alikuwa amekiuka katiba ya Chadema, ndipo mwaka 2015
akafukuzwa uanachama na baadaye akajiunga na chama cha ACT-Wazalendo.
Ndani
ya Chadema, Zitto Kabwe anatafsiriwa kama msaliti ambaye alikuwa
anakihujumu chama. Kwa Chadema, Zitto, Profesa Kitila Mkumbo na
aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba,
walitajwa kuwa wasaliti na walikihujumu chama hicho. Mtazamo wa Chadema
ulijengwa zaidi na matukio yote ambayo yalisababisha malumbano ndani ya
chama, hata kama yalikuwa ya kidemokrasia. Hujuma yao kubwa ilitajwa
kuandaa mkakati wa ushindi ambao ungemwondoa Mbowe madarakani kupitia
sanduku la kura.
Ndani
ya chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe alikuwa na washirika wake wa
karibu, Profesa Kitila Mkumbo, Samson Mwigamba na wakili maarufu Alberto
Msando. Zitto alijiunga ACT- Machi 20, 2015 na kukabidhiwa kadi na
Mwenyekti wa Tawi la Tegeta.
Cha
kustaajabisha ni kwamba, Zitto amekimbiwa na washirika wake ndani ya
chama kutokana na sababu mbalimbali, ikiwamo kutoeleweka kwa miongozo ya
Kiongozi Mkuu wa Chama (Party Leader).
Profesa
Kitila Mkumbo aliteuliwa na Rais John Magufuli kuwa Katibu Mkuu wa
Wizara ya Maji. Kitila alikuwa mshauri wa ACT-Wazalendo na mshirika wa
karibu wa Zitto kwa muda mrefu. Kitila na Zitto walifukuzwa pamoja ndani
ya Chadema sambamba na aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Arusha,
Samson Mwigamba.
Aliyekuwa
mwenyekiti wa chama hicho, Anna Mghwira, ameteuliwa na Rais Magufuli
kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro. Mara baada ya uteuzi huo, chama cha
ACT-Wazalendo kilitangaza kumwengua katika nafasi yake ya uenyekiti.
Sasa
hali imekuwa mbaya zaidi, kwani Samson Mwigamba ambaye alikuwa Kiongozi
wa Kamati ya Uchaguzi ya chama hicho, naye amemkimbia Zitto Kabwe na
kujiunga na Chama Cha Mapinduzi – CCM.
Mwigamba
amekimbilia CCM ambako aliwahi kukibeza na kuishambulia kwa lugha kali
ambazo baadhi zilimfikisha mahakamani kwa madai ya kuwachochea askari
kuasi. Awali Mwigamba alijiuzulu wadhifa wake wa Katibu Mkuu kwa sababu
alikuwa akielekea masomoni na kufanya kazi mjini Arusha katika Chuo
Kikuu cha Kenyatta.
Sasa Mwigamba amekikimbia ACT-Wazalendo na kwenda CCM, huku akiacha shutuma mbalimbali dhidi ya viongozi wenzake.
Uamuzi
wa Mwigamba ulitokea siku chache baada ya Profesa Kitila Mkumbo kujivua
uanachama wa ACT-Wazalendo, kwa madai anashindwa kuaminiwa na
kutekeleza vizuri majukumu yake ndani ya wizara kwa kudhaniwa kuwa
mpinzani.
“Mnamo
Aprili 25, 2016, nilipokuwa nang’atuka ukatibu mkuu, nilipotoa nasaha
zangu mbele ya wajumbe wa Halmashauri Kuu ya chama nilisema, salama ya
chama chetu ni kubaki kwenye misingi ya uanzishwaji wake.
“Hii
haikuwa bahati mbaya, bali nilimaanisha kwa kuwa nilishaanza kuona
mwelekeo wa baadhi ya viongozi kuchepuka nje ya misingi ya chama. Na
kutokea hapo nimekuwa nikiwalalamikia sana viongozi juu ya kuacha
misingi na mambo ya msingi yaliyotufanya tuanzishe chama hiki, mara
nyingine nikifikia kutofautiana sana hata na wewe binafsi (Kiongozi Mkuu
wa Chama).
“Kwa
kuwa hali hiyo kwa sasa inazidi kuongezeka na jambo ambalo binafsi
naamini ndiyo sababu hasa ya Prof Kitila Mkumbo kujivua uanachama,”
ilisema barua ya Mwigamba kwenda kwa Kiongozi Mkuu wa Chama, Zitto
Kabwe.
Swali
la kujiuliza hapa je; Zitto Kabwe amesalitiwa na washirika wake au yeye
amewasaliti? Kwa sababu washirika wake wamekuwa wakilalamika, huku yeye
akiwa ndiye kiongozi mwenye sauti ya mwisho ndani ya chama.
Hii
inaleta mantiki juu ya malalamiko ya Chadema kuwa mwanasiasa huyo
alikuwa akikihujumu chama, na sasa anakiongoza chama ambacho yeye ndiye
taswira kuu, huku wengine wakikosa umuhimu.
Udhaifu huu umechochea
ACT-Wazalendo kuonekana kama chama cha mtu mmoja na kufifisha umahiri wa
wengine.
chanzo:Mpekuziblog.
Comments