
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi mjini Chake Chake, Mdhamini
wa Mamlaka hiyo Pemba, Suleiman Ame Juma amesema, mashamba hayo
waliyafichua baada ya watendaji wake kufanya uchunguzi wa kina, wa
mashamba hayo ya mikarafuu.
Alisema kuwa, baada ya kufanya uchunguzi huo, walibaini kwamba jumla
ya shilingi milioni 84,700,000 zingepotea na kuishia mikononi mwa
wachache, ingawa walifanikiwa kuziokoa, kutokana na kufichwa kwa
mashamba 30 ya eka tatu tatu ya Serikali, katika maeneo tofauti ya
kisiwani Pemba.
“Zaidi ya mashamba 30 ya mikarafuu ambayo yalionekana kama sio ya
serikali, lakini baada ya uchunguzi wetu tumeyabaini, kwamba ni ya
serikali na tumefanikiwa kuziokoa fedha hizo baada ya kukodishwa”,
alisema Suleiman.
Alifafanua kuwa, kuna mashamba yamekuwa yakifichwa na baadhi ya
watendaji au watu wa kawaida, na kuonekana kama sio ya serikali, ambapo
watendaji mbali mbali serikalini, hutumia mwanya huo kwa kuyatumia wao,
jambo ambalo ni kosa kisheria.
“Kwa kweli mashamba yanafichwa kwa lengo la kuyatumia kwa shughuli
zao binafsi, lakini tutaendelea kuchunguza, ili kuondoa suala zima la
uhujumu wa uchumi, kama moja ya kazi zetu”,aliongeza.
Alieleza kuwa, kama hadi sasa Wizara husika imeshaingiza shilingi
milioni 900.661, kwa ukodishaji wa mashamba ya serikali, basi mchango wa
ZAECA, baada ya kuyaibua mashamba hayo 30 kati ya 1,451, ni shilingi
miloni 84.7, ni mchango wetu.
Alisema walizipata taarifa hizo, baada ya kuhojiana na wananchi na
wengine kufika ofisini kwao kutoa taarifa, juu ya uwepo wa mashamba ya
mikarafuu ya serikali, kwenye maeneo ambayo zoezi limeshapita.
Tayari mashamba ya mikarafuu ya eka tatu tatu 1,451 yameshakodishwa
na wizara ya Kilimo, Maliasiali, Mifugo na Uvuvi Pemba, na laiti kama
waliokodi wengeshalipa fedha zote hizo, serikali ingejipatia wastani wa
zaidi ya shilingi bilion 2.393.
Ingawa hadi sasa kati fedha hizo ziliotarajiwa kupatikana, hadi
Oktoba 17, ni shilingi bilioni 1.492 zilizokuwa hazijalipwa na wananchi
mbali mbali waliokodi mashamba ya mikarafuu ya Serikali kisiwani Pemba.
Zoezi la ukodishaji wa mashamba ya mikarafuu kisiwani Pemba, lilianza
mwezi Julai mwaka huu, ambapo jumla ya mashamba 1,451 yalishakodishwa,
kati ya mashamba 1,525 yaliotarajiwa kuibuliwa kabla ya kuanza kwa zoezi
la ukodishaji.
chanzo: zanzibar24.
Comments