
Ushauri huo umetolewa na Naibu Waziri wa Afya Harusi Said Suleiman alipokuwa akifungua mkutano mkuu wa uchaguzi wa Jumuiya ya wauguzi Zanzibar (ZANA) katika Chuo Maendeleo ya Utalii Maruhubi.
Aliwaeleza wauguzi na wakunga kwamba katika kukabiliana na mabadiliko makubwa ya sayansi na teknonlojia duniani wanahitaji kuwa na taaluma ya hali ya juu ya maswali ya kada zao ili kuweza kukabiliana na changamoto mbali mbali zinazowakabili.
Alisema hivi sasa malalamiko ya wananchi juu ya wauguzi na wakunga yameanza kupungua lakini wanahitaji kuongeza juhudi kuhakikisha lawama zinazotolewa na wananchi zinaondoka kabisa.
Naibu Waziri aliwataka kuongeza ushirikiano na kutoa huduma sawa kwa watu wote bila ya kuangalia jinsia, itikadi ya kisiasa na wenye uwezo na wasio na uwezo na kuakikisha wanatumia lugha nzuri kwa wagonjwa na wasaidizi wao wakati wa kuwahudumia.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wauguzi Zanzibar Valeria Rashid Haroub ameiomba Wizara ya Afya na Wizara ya Elimu kuhakikisha vyuo vyote vinavyotoa taaluma ya Uuguzi na Ukunga kuhakikisha vinachukuwa wanafunzi wenye sifa na kwa idadi inayokubalika na Baraza la wauguzi.
Aidha walivitaka vyuo vyote kufuata viwango vilivyowekwa kisheria ili kutowa wauguzi bora na kupunguza malalamiko katika jamii.
Katika risala yao iliyosomwa na Said Mohd Salum walisema Jumuiya ya ZANA inalengo la kuinua hadhi ya wauguzi na wakunga pamoja na taaluma yao ili waweze kutoa huduma bora kwa wagonjwa na wenye kuhitaji msaada wao.
Walisema katika tafiti zilizofanywa katika siku za karibuni zimeonyesha kuwa zaidi ya asilimia 80 ya wananchi waliohojiwa wameeleza kuridhishwa na huduma wanazopata wanapofika hospitali na vituo vya afya.
Hata hivyo walisema kuwepo muundo wa utumishi unaopelekea utaratibu usioridhisha katika nyongeza za mishahara na tafauti iliopo baina ya mishara ya wauguzi na wakunga ukilinganisha na madaktari ni moja ya tatizo linalosababisha kupunguza ari ya utendaji.
Walieleza kuwa kukosekana kwa bima ya afya kunapelekea wauguzi, wakunga na familia zao wanapopata matatizo ya afya kukosa pakukimbilia na hatimae hubeba mzigo mzito wasioweza kuumudu ni changamoto inayowakabili hadi hivi sasa.
Jumuiya ya Wauguzi Zanzibar inafanya uchaguzi wa viongozi wapya watakao ongoza kwa kipindi cha miaka mitatu ambapo Mwenyekiti wa sasa Valeria Rashid Haroub anagombea kwa mara nyengine nafasi hiyo.





chanzo:zanzibar24.
Comments