Mwamko mkubwa wa kufanya mazoezi unaonekana sehemu nyingi za Zanzibar
bado haujasaidia sana kupunguza maradhi yasioambukiza na hatimae
maradhi hayo yanaendelea kuwasumbua wananchi wengi.
Meneja wa kitengo cha maradhi yasiyoambukiza Omar Mwalimu alisema
hayo kwenye mhadhara wa wazi wa wanafunzi wa vyuo vikuu ulioandaliwa na
Mtandao wa Kimataifa wa wananfuzi wa Zanzibar uliofanyika Chuo Kikuu cha
Zanzibar Kempasi ya Mpendae.
Alisema kufanya mazoezi ni moja ya sababu ya kupunguza kuongezeka
maradhi yasiyoambukiza lakini tatizo ni chakula bora chenye mchanganyiko
wa vitu mbali mbali kimekuwa kikikosekana kwa wananchi wengi.
Alisisitiza kuwa kufanya mazoezi kila siku ni jambo la msingi katika
kuimarisha afya za wananchi lakini kuwa muangalifu katika matumizi ya
chakula cha kila siku ni kitu muhimu zaidi katika kupambana na maradhi
yasiyoambukiza.
Meneja huyo aliwashauri wananchi kubadili tabia na kuwataka kutumia
matunda na mboga kwa wingi na kupunguza chakula chenye vichocheo vya
kupata maradhi yasiyoambukiza ambayo yamekuwa yakiuwa watu wengi zaidi
hivi sasa duniani.
Meneja wa Jumuiya ya Muungano wa Maradhi yasiyoambukiza Zanzibar
Zuhura Saleh Amour alisema kisukari ambayo ni moja ya maradhi
yasiyoambukiza yamekuwa yakipoteza maisha ya wananchi wengi duniani na
nchi zinazoathirika zaidi ni nchi zinazoendelea.
Aliwataka wanafunzi wa vyuo vikuu na wananchi wa kawaida kujenga
utamaduni wa kupima afya zao mara kwa mara kwani maradhi hayo yanachukua
muda mrefu kugundulika kama mtu hajapima afya yake.
Aliwashauri kuacha kutumia bidhaa zinazotokana na tumbaku kwa vile
imegundulika kuwa matumizi ya tumbaku ni miongoni mwa mambo
yanayohatarisha kupata maradhi yasiyoambukiza.
Aidha alisisitiza umuhimu wa kuweka mbele kujikinga na maradhi hayo kwani
yanapokupata matibabu yake yanakuwa magumu na yanachukua muda mrefu
kuondoka.
Akifungua mkutano huo, Afisa wa kitengo cha maradhi hayo Omar Abdalla
alisema Zanzibar imeongeza maradhi ya homa ya ini, maradhi ya kinywa na
ajali kuwa ni miongoni mwa maradhi yasiyoambukiza.
Alisema maradhi hayo mapya na yale maarufu ya sinikizo la damu,
saratani, kisukari na maradhi yanayoambukiza kwa njia ya hewa yanachukua
asilimia 43 ya vifo vyote vinavyotokea Zanzibar.
Wanafunzi walioshiriki mhadhara huo walikishukuru kitengo cha maradhi
yasiyoambukiza kwa kuwapa taaluma kubwa ambayo imewawezesha kujuwa
sababu na njia ya kujikinga na maradhi hayo.
Waliahidi kuwa watakuwa walimu wazuri wa kuwaelimisha wananchi
wenzao na kuwa mfano wa kuigwa na wananchi wengine katika sehemu
wanazoishi ili kuona wanajikinga na maradhi hayo.
![]() |
![]() |
![]() |
![]() |
![]() |
chanzo:zanzibar24.
Comments