Rais
John Magufuli amesema atashangaa sana kuona fedha alizoidhinisha kwa
ajili ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu, hazitawafikia walengwa kwa
wakati.
Katika
hatua nyingine Rais, Magufuli ameagiza kufanyika kwa mabadiliko ya
haraka katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
ili wizara hiyo iweze kujiendesha kwa kuzingatia diplomasia ya uchumi,
kama chachu ya utekelezaji wa sera ya viwanda.
Alisema
hayo Ikulu jijini Dar es Salaam juzi mara baada ya kuwaapisha Makatibu
Wakuu, Naibu Makatibu Wakuu, Wakuu wa Mikoa na Mabalozi, aliowateua,
tukio lililoambatana na viongozi hao kula kiapo cha maadili.
Rais
Magufuli alisema mwezi uliopita Wizara ya Fedha na Mipango ilitoa Sh
bilioni 147 zilizoidhinisha kwenda Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia
na Mafunzo ya Ufundi kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu
wanaostahili kupata.
“Nitashangaa
sana kama patakuwepo wanafunzi waliopo kwenye orodha ya kupata mikopo
na wawe hawajapata, nitashangaa sana kwa sababu mimi najua
nimeshaidhinisha fedha hizo na zimeshatoka,” alisema Rais Magufuli.
Alisema
anayasema hayo kwa sababu inaweza kutokea wanafunzi wakafungua vyuo na
kuanza kuhangaika vyuoni bila kupata mikopo, jambo ambalo alisema hataki
kulisikia.
“Ndiyo
maana wakati mwingine nalazimika kuwaza kuwa fedha zimewekwa benki
kwenye fixed deposit (akaunti ya muda maalumu) zinamzalishia mtu,”
alisema.
Aliwataka
pia viongozi hao walioapishwa, kuzingatia sheria katika utekelezaji wa
majukumu yao na pia wakawe watumishi wa watu hasa watu wanyonge.
“Ninyi
ni wawakilishi wa Watanzania, mkawe sauti na wasemaji wao,
mkamtangulize Mungu katika kuwahudumia, mkizingatia hayo mtaweza kujibu
hoja za Watanzania,” alisema Rais Magufuli.
Aliwataka viongozi katika ngazi zote, kuangalia vitu ambavyo wanaweza kufanya kuleta mabadiliko ya kiuchumi kwa wananchi wao.
Aidha,
Rais Magufuli alisema ameamua kufanya mabadiliko katika Wizara ya Mambo
ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ili kuleta matokeo ya haraka,
kuendana na Tanzania ya Viwanda.
Alisema
ili kuifanya wizara hiyo kuendana na diplomasia ya kisasa inayoegemea
katika uchumi, ndiyo maana ameamua kumteua Profesa Adolf Mkenda ambaye
ni mchumi kushika nafasi ya Katibu Mkuu ya wizara hiyo ili kuwa chachu
ya mabadiliko ya kiuchumi.
Kabla
Profesa Mkenda alikuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na
Uwekezaji. Alisema anataka kuona kila balozi katika nchi anayowakilisha,
anakuwa sehemu ya ukuaji wa uchumi wa Tanzania na kwamba kuanzia sasa
kila baada ya muda fulani, kila balozi ataeleza ameiletea nchi uwekezaji
gani.
Alitaka
pia kuwepo kwa mfumo maalumu wa kuwachagua watumishi wa serikali wenye
uwezo kufanya kazi katika wizara hiyo, kwa vile hivi sasa kuna tabia
watumishi wasiofaa serikalini, ndiyo wanapelekwa katika wizara hiyo
kupumzika na wengine kupelekwa katika balozi mbalimbali wakiwa hawana
uwezo.
Alisema
balozi za Tanzania katika nchi mbalimbali, zina watumishi wengi kuliko
uhitaji, tofauti na balozi za nje nchini ambazo zina watumishi wa nchi
hizo wachache na wanaajiri Watanzania kutekeleza majukumu mengine na
kuleta ufanisi. Alimtaka Profesa Mkenda kuangalia dhana hizo.
Katika
hatua nyingine, Rais Magufuli alisema aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya
Dodoma Mjini ambaye sasa amemteua kuwa Mkuu wa Mkoa, Christina Mndeme
atakuwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma na kubadilishana na Mkuu wa Mkoa huo, Dk
Bilinith Mahenge ambaye sasa atahamia Dodoma.
Katika
hatua nyingine Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan amewaagiza Mawaziri,
Naibu Mawaziri na Makatibu Wakuu kufika katika Studio za Televisheni ya
Taifa (TBC), kueleza mafanikio ya serikali kama ilivyopangwa.
“Mawaziri,
Naibu Mawaziri na Makatibu Wakuu, TBC imetayarisha vipindi maalumu vya
kuelezea mafanikio tuliyoyafikia katika miaka hii miwili, lakini
kumekuwa na kukimbiakimbia kwenda kueleza mafanikio ya serikali kwa
wananchi.
"Naomba
niseme hapa, Mawaziri wote wanatakiwa kushiriki kwenye vipindi hivi.
Kwa wale ambao ni wapya wapo Makatibu wakuu na watendaji wengine
wanaofahamu nini kimefanyika kwenye wizara zao, wawasaidie mawaziri
kufanikisha hili,” alisema Samia.
Aliwataka
Makatibu Wakuu, Naibu Makatibu Wakuu, Wakuu wa Mikoa na Mabalozi
walioteuliwa kwenda kuwa watumishi wa watu badala ya kuwa watawala na
aliwataka wafikiri kwanza kabla ya kuamua jambo wanalolifanyia uamuzi
ili kulinufaisha taifa.
Spika
wa Bunge, Job Ndugai mbali ya kuwapongeza viongozi hao walioapishwa
alisema dhamana waliyopewa ni kubwa na kwamba matarajio ya wananchi kwao
ni makubwa.
Jaji
Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma, alisema wakuu wa mikoa ni wadau
muhimu katika sheria, kwani ni wenyeviti wa Kamati za Maadili za Mikoa
na hivyo wana wajibu wa kusimamia maadili ya viongozi wote mikoani mwao.
chanzo:Mpekuziblog.
Comments