Hata hivyo, kuna upinzani mkali katika kaunti ambazo ni ngome ya Odinga likiwemo eneo lote la Nyanza. Huko, viongozi wa dini na siasa wamejitokeza leo kuitaka Tume ya Uchaguzi iahirishe uchaguzi uliopangwa kufanyika kesho ili kuepusha madhara.
Wakizungumza na wanahabari asubuhi leo kwenye kanisa la St Stephens ACK mjini Kisumu, viongozi hao wamesema kura iliyopangwa kufanyika katika kaunti nne mpakani mwa Nyanza inaweza kusababisha machafuko na ukatili wa polisi.
Viongozi hao wametoa wito pia kuondolewa kwa maofisa usalama katika eneo la Nyanza na wakamtaka Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati kuondoa maboksi ya kura na kurudisha Nairobi.
Watumishi wa Mungu waliotoa wito huo ni Joshua Owiti wa dayosisi ya Maseno Mashariki, Francis Mwai Abiero (akofus mstaafu wa dayosisi ya Maseno Magharibi), Profesa David Kodia (Bondo), Askofu mkuu Habakuk Abogno (Kanisa la Kristo Afrika) na Askofu Betty Onyango (Kanisa la Tisa la Afrika).
"Kwa Bwana Chebukati kusema kwamba amemuomba Joseph Boinnet (IGP) kwa msaada zaidi ili kuhakikisha upigaji kura hasa kaunti za Siaya, Kisumu, Homa Bay na Migori unafanyika ni leseni kwa vikosi vya serikali kuua watu kwa sababu lugha pekee ambayo Boinnet anaijua ni bunduki na risasi," alisema Kasisi Joshua Owiti.
Vurugu Migori
Viongozi hao wametoa kauli hiyo huku waandamanaji wakiongeza juhudi za kuhakikisha uchaguzi wa marudio kwa kura ya urais haufanyiki katika kaunti ya Migori kama ulivyopangwa na maofisa uchaguzi wa Nyanza.
Baada ya maandamano ya Alhamisi, wengine walikesha usiku kucha wakipanga mawe na kuwasha moto katika lango la kuingilia na kutoka kaunti hiyo ya mpakani kwa barabara.
Katika juhudi hizo walikwenda mbali zaidi hadi kufikia kutandika nondo na kuchomelea kuzuia barabara inayotoka Migori kwenda hadi Tanzania ili isiwe rahisi kwa maofisa wa IEBC kupeleka vifaa vya uchaguzi.
Halafu vijana waliungana katika makundi wakiwa na silaha na kulinda vizuizi hivyo ili magari yabadili uelekeo. Barabara nyingine iliyowekewa vizuizi ni ya kutoka Kisii kwenda Awendo.
Masanduku
Mmoja wa maofisa waliotekeleza masanduku ya kura na kuzima simu alikamatwa Magarini, kaunti ya Kilifi. Polisi wa Magarini walifanikiwa kumfuatilia na kumtia ndani kwa kutoroka kazi.
Mkuu wa kituo cha polisi cha Magarini Gerald Barasa alisema alimkamata Nicholas Surei, aliyekuwa ofisa msimamizi katika kituo cha Kwa Ndomo na akatelekeza masanduku katika kituo cha kujumlishia cha Chuo cha Ufundi cha Mapimo.
Maofisa wengine wanne walichelewesha kutangaza matokeo katika kituo cha Chuo cha Ualimu cha Shanzu jimbo la Kisauni baada ya kutelekeza masanduku na kuzima simu.
chanzo:Mwananchi.
Comments