
Polisi wamesema baada ya kuwapekuwa, watuhumiwa hao walikutwa na
mabomu saba, SMG moja ikiwa imefutwa namba zake na ‘magazine’ moja ndani
yake ikiwa na risasi 16, maganda 10 ya SMG na pikipiki aina ya Fekon.
Kamanda wa Kanda hiyo, Lazaro Mambosasa, aliwaambia waandishi wa
habari jijini jana kuwa tukio hilo lilitokea usiku wa Jumatatu maeneo ya
Msongola wilayani Ilala.
Mambosasa alisema askari wake wakiwa katika doria ya kusaka
watuhumiwa wa mauaji ya Kibiti, walitilia shaka pikipiki iliyokuwa
imebeba watu watatu ikiwa haina namba.
“Polisi walianza kuifuatilia na walipogundua kuwa wanafuatiliwa
waliongeza mwendo na kukatisha njia kuingia barabara ya vumbi na
walianza kufyatua risasi na polisi walijibu mashambulizi na kuwajeruhi,”
alisema.
Kamanda Mambosasa alisema baada ya watuhumiwa hao kupigwa risasi walianguka na pikipiki yao.
“Katika upekuzi, watu hao walikutwa na silaha aina ya SMG moja ikiwa
imefutwa namba zake na magazine moja ikiwa na risasi 16, maganda 10 ya
SMG, mabomu aina ya Graned saba na pikipiki moja aina ya Fekon,” alisema
Kamanda Mambosasa.
Aliongeza kuwa watu hao ambao wanakadiriwa kuwa na umri kati ya miaka
30 hadi 40 hawakutambuliwa majina yao na juhudi za kuusaka mtandao
waliokuwa wakishirikiana nao zinaendelea.
Alisema watuhumiwa hao walipofikishwa Hospitali ya Temeke, daktari wa
zamu siku hiyo alithibitisha walikuwa wameshafariki dunia na miili yao
imehifadhiwa hospitalini hapo.
Katika tukio lingine, Kamanda Mambosasa alisema wamewaua watuhumiwa
wengine wawili wa ujambazi eneo la Kibonde Maji, Mbagala Zakheim jijini
Dar es Salaam.
Alisema watuhumiwa hao waliuawa Jumamosi usiku wakati askari wakiwa
katika doria na kupata taarifa kuwa kuna majambazi wamepanga kupora
katika maduka ya M-Pesa na Tigo-Pesa.
“Polisi walifika mapema na kuweka mtego wao ndipo ilipofika saa mbili
usiku watuhumiwa walikuja na pikipiki moja ikiwa haina namba wakiwa
wamebebana watatu,” alisema.
Kamanda Mambosasa aliongeza kuwa wawili kati yao walishuka na
kumuacha mmoja kwenye pikipiki ambaye alidai ndiye aliyekuwa dereva wao.
Alisema askari walipowafuata ili wawakamate, dereva wa pikipiki
alishtuka na kukimbia na mmoja wa majambazi alichomoa bastola na
kufyatua risasi ndipo polisi walipojibu mapigo.
Alisema polisi waliwashambulia kwa risasi na kuwajeruhi watuhumiwa
wawili ambao baada ya upekuzi walikutwa na bastola ikiwa na magazine
yake na risasi moja na maganda matano ya risasi.
Alisema silaha hiyo ilikuwa imepakwa rangi nyeusi ili kuficha
utambuzi wa aina ya silaha hiyo, lakini uchunguzi umebaini kuwa ni
bastola aina ya CZ ambayo imefutwa namba zake.
Alisema watu hao walifariki dunia na miili yao imehifadhiwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) ikisubiri kutambuliwa.
Kamanda Mambosasa pia alisema wanawashikilia watu tisa akiwamo raia
wa Yemen ambao wanadaiwa kujihusisha na vitendo mbalimbali vya uhalifu.
Alisema watuhumiwa hao walikamatwa maeneo ya Magomeni Mikumi baada ya kupokea taarifa ya kuwapo kwa mtandao huo.
Alisema watuhumiwa hao walikutwa na magari mawili wanayodaiwa kuwa ni
ya wizi, mirungi bunda sita, simu 100, kompyuta mpakato tatu huku mmoja
wao akibainika ni mhamiaji haramu.
Kamanda Mambosasa alisema watuhumiwa hao walikutwa na magari mawili
yanayohisiwa kuwa ni ya wizi na ndani ya magari hayo kulikutwa na namba
za bandia ambazo ni T 937 DJE aina Toyota IST rangi ya bluu bahari na T
774 DHY ambazo gari lake halikufahamika.
Alisema ndani ya gari hilo kulikutwa simu 100, kompyuta mpakato tatu
na nyaya mbalimbali na kwamba gari jingine lilikutwa na namba za bandia
ambazo ni T 375 CQP aina ya Toyota Vits rangi ya fedha.
Kamanda Mambosasa alisema katika mahojiano na watuhumiwa hao,
ilibainika mmoja wao aitwaye Osman Ahmed (25) ni raia wa Yemen ambaye
anaishi nchini bila kibali.
chanzo: zanzibar24.
Comments