Mkuu
wa Mkoa wa Tanga, Martine Shigella amempa siku mbili Mkurugenzi
Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto, Kazimbaya Makwega
kuhakikisha anawasilisha taarifa ya ujenzi wa darasa la Shule ya Msingi
Mkundiambaru.
Hatua hiyo inatokana na kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kukataa kulizindua baada ya kubainika limejengwa chini ya kiwango.
Agizo
hilo amelitoa leo Jumanne katika Uwanja wa Ndege wa Tanga baada ya
kiongozi huyo wa mbio za Mwenge, Amour Hamad Amour kueleza akiwa
wilayani Lushoto Septemba 22 aligoma kuzindua darasa hilo kutokana na
kuwepo dosari kuu tatu.
Akizungumza
wakati akiwaaga viongozi wa Mkoa wa Tanga kuelekea Kusini Pemba leo,
Amour amezitaja dosari hizo kuwa ni darasa dogo lisilokidhi vigezo, lina
nyufa na limeezekwa kwa mabati ya geji 32 badala ya 28 zinazotakiwa
kwenye majengo ya Serikali.
“Tukiwa
Lushoto nilimwagiza kabla ya kuondoka Tanga leo awe ameniletea Bill of
Quantities –BOQ (mchanganuo wa makadirio ya kazi) na hati ya ununuzi wa
vifaa vya mradi lakini nasikitika kuwa hajaleta. Kwa hiyo, nampa siku
nne awe ametuletea Pemba ili tuweze kupeleka taarifa kwa viongozi wetu,”
amesema Amour.
Darasa hilo lilipangwa kuzinduliwa wakati wa mbio za Mwenge wa Uhuru wilayani Lushoto.
Makwega
katika taarifa baada ya Amour kugoma kulizidua jengo hilo alieleza
lilijengwa kwa nguvu za wananchi waliotumia Sh7 milioni badala ya Sh11
milioni zilizohitajika.
Kuhusu mabati alisema yameezekwa ya muda na kwamba, uongozi wa halmashauri umepanga kuyaondoa na kuezeka mengine.
Majibu
hayo hayakumridhisha Amour aliyemuagiza kuwasilisha BOQ na hati ya
ununuzi wa vifaa vya mradi huo kabla Mwenge haujakabidhiwa Kisiwani
Pemba.
“Hadi
leo tumepita mikoa 26, mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto
ndiye aliyetukwaza, tulimwagiza kabla hatujatoka Tanga awe ameleta
taarifa ya darasa hilo lakini hadi sasa Oktoba 3 hatujamuona. Tunakuomba
RC mweleze kuwa awe ameleta ndani ya siku nne tutakazokuwa Pemba,”
amesema Amour.
Mkuu wa mkoa, Shigella amesema atahakikisha taarifa hiyo inawasilishwa kwa kiongozi huyo kesho Jumatano.
“Wewe umetoa siku nne, mimi namwagiza kesho awe ameshawasilisha taarifa hiyo,” amesema Shigella.
chanzo:Mpekuziblog.
Comments