
Masheha wa shehia hizo Pemba, wamesema kama wakiongezewa nguvu kwenye
shehia zao, ili kuwazuia moja kwa moja wanawake na watoto
wanaojihusisha na uokotaji mpeta, watajenga nguvu nzuri ya kufanikisha
suala hilo.
Wakizunguma na mwandishi wa habari hizi, masheha hao walisema
walishatoa elimu ya kutosha, juu ya kuwakataza kuokota mpeta, ingawa
wapo wanaoendelea kupuuzia agizo hilo.
Sheha wa shehia ya Mwambe Hamad Haji Faki alisema sio vibaya kama
serikali ya wilaya, italiingilia kati hilo, kwa kushirikiana na wao, ili
kuwadhibiti wale wanaopinga agizo la serikali za shehia, wilaya, Mkoa
na taifa.
Alisema ameshajaribu kuyatumia makundi mbali mbali ndani ya shehia
yake, kama vile polisi jamii, wazazi, walezi, waalimu wa madrassa na
waalimu wa skuli, ili kuwaelimisha wananchi ingawa bado hali ni tete.
Nae sheha wa shehia ya Jombwe Hakim Khamis Omar, alikiri kuwa shehia
yake nayo inayo wananchi, wanaoendelea kupuuzia agizio la serikali,
hivyo lazima sasa asaidiwe nguvu.
“Polisi jamii wapo, jamii ipo lakini suala la kuokota mpeta wapo
wanaoona kama hakuna marufuku yoyote ya kuokota mpeta, maana wamekuwa,
wakitoka makundi kwa makundi”,alisema.
Nae sheha wa shehia ya Chambani Mohamed Abdalla, alikiri kuwa, wapo
wananchi wanaoendelea kupuuzia agizo hilo, ingawa alishakaa nao muda
mrefu, kuwaeleza na kuwakataza.
“Mimi nishakaa na wananchi wangu, na kuwaeleza wananchi wote kuwa,
agizo la serikali kuu ni uwepo wa marufuku wa kuokota mpeta, ingawa bado
wanakwenda kwa wingi”,alifafanua.
Baadhi ya wananchi wa shehia hizo, walisema hakuna uhusiano baina ya
uwepo wa zao la karafuu na udhalilishaji, hasa kwa vile zipo kesi
zilizowahi kuripotiwa, kabla ya kuanza kwa msimu huu.
Mwanakhamis Haji Mcha, alisema kisingizio cha mpeta kuchangia ubakaji
na udhalilishaji sio sahihi, kwa vile mwenye tabia hiyo hawezi kukaa
kwa kusubiri karafuu.
“Kama kuna mwanamke anafanya matendo machafu, huyo ni tabia yake hata
karafuu zikimalizika, basi atendelea, maana mtu na tabia yake huwa ni
kama ngozi”,alisema.
Hassina Shehe Jaku, alisema wanachojikinga wao kwenye mashamba ya
mikarafuu, ni kukatazana kuiba karafuu za watu, na kutoingia kwenye
mashamba, mwenye aliopiga marufuku.
Kwa upande wake Subira Haji Vuaa, alisema sio rashisi kufanya matendo
machafu kwenye mashamba ya mikarafuu, kwa huwepo makundi makubwa ya
watu.
Wakati huo huo, uongozi wa Polisi jamii shehia za Mwambe, Jombwe
wamefanikiwa kuwazuia wanawake na watoto kutotoka majumbani mwao baina
ya saa 10: 00 na 10:30 alfajiri, kwenda kwenye uokotaji mpeta na
kutakiwa kuanza kuondoka saa 12:00.
Mkuu wa wilaya ya Mkoani Hemed Suleiman Abdalla, aliendeela kutoa
tamko la kuwataka wanawake na watoto kuacha kwenda kuokota mpeta, kwani
matendo ya udhalilishaji huchukua nafasi.
chanzo: zanzibar24.
Comments