Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan amezindua makumbusho ya Olduvai Gorge, ambako ni chimbuko la historia ya binadamu.
Amesema makumbusho hayo ni kielelezo cha maisha na ustaarabu wa binadamu ambao unaelezea maisha ya vizazi vilivyopita.
Amesema ujenzi wa makumbusho hayo utasaidia kuvutia watalii na wanasayansi wa masuala ya mambo kale duniani.
Samia
amesema eneo la Ngorongoro lina historia kubwa ya maisha ya zamadamu
ikibainika miaka 3 milioni iliyopita walikuwepo walioishi kwa kutembelea
miguu miwili.
Amesema
eneo la Ngorongoro kumebainika miaka 2.7 milioni iliyopita binadamu
walianza kutumia zana za mawe katika kula nyama na kuwinda.
“Hapa ni chimbuko la historia ya zamadamu, Serikali itaendelea kulihifadhi na kulitunza eneo hili,” amesema.
Makamu wa Rais ameishukuru Jumuiya ya Ulaya kwa kutoa fedha kugharimia ujenzi wa makumbusho hayo na miundombinu yake.
Makamu
wa Rais ameitaka Wizara ya Maliasili na Utalii na Mamlaka ya Hifadhi ya
Ngorongoro kuwa na mkakati wa kutangaza makumbusho hayo ndani na nje ya
nchi ili kuvutia zaidi watalii.
Pia,
amewaomba wananchi wa Ngorongoro kuendelea kuhifadhi eneo hilo ikiwemo
kutopeleka mifugo eneo la Creta. Amesema Serikali inajitahidi
kuwaondolea kero zao likiwemo tatizo la maji.
Awali,
Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe alisema eneo la
Ngorongoro ni la urithi wa dunia, hivyo wizara kwa kushirikiana na
mamlaka wataendelea kulihifadhi na kulitunza.
Naibu
Mhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, anayeshughulikia huduma
za jamii, Asangye Bangu amesema ujenzi wa makumbusho hayo utasaidia
kuongeza watalii.
Ametoa wito kwa mawakala wa utalii kuwapeleka watalii eneo la Olduvai Gorge ili kuongeza mapato kwa manufaa ya Taifa.
Meneja
wa idara ya urithi wa tamaduni katika Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro,
Mhandisi Joseph Mwankunda amesema ujenzi wa eneo hilo umegharimu Sh1.7
bilioni.
Amesema makumbusho hayo ni ya kisasa zaidi duniani na wanatarajia yatadumu kwa zaidi ya miaka 50.
Meneja
miradi katika Jumuiya ya Ulaya, Alexa Haden amesema jumuiya ya Ulaya
imetoa fedha katika mradi huo kutokana na kuthamini mchango wa mambo ya
kale.
Akizungumza
katika hafla hiyo, Mbunge wa Ngorongoro, William ole Nasha ameomba
mafanikio ya mradi huo kugusa maisha ya wananchi wanaoishi ndani ya
mamlaka hiyo wanaokabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo upungufu wa
maji.
chanzo:Mpekuziblog.
Comments