Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Magufuli amewatahadharisha watendaji wa Wizara ya Elimu kuhakikisha wanatoa mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu wenye sifa ya kupata mikopo kabla ya vyuo kufunguliwa.
Akizungumza mara baada ya kuwaapisha viongozi mbalimbali aliowateua Ikulu jijini Dar es Salaam leo Ijumaa, Magufuli amesema imekuwa kawaida vyuo kufunguliwa wakati wanafunzi wanaopaswa kupewa mikopo hawajapewa jambo ambalo hufanya maisha ya wanafunzi hao kuwa magumu.
Serikali imetoa Shilingi147 bilioni kwa ajili ya wanafunzi wenye sifa ya kupata mkopo katika mwaka mpya wa masomo unaotarajia kuanza mwezi ujao wa Novemba.
“Tarehe 29 mwezi uliopita wizara ya fedha imetoa Shilingi bilioni 147, zimepelekwa Wizara ya Elimu, ni mikopo ya wanafunzi wenye sifa, nitashangaa kama watakuwepo wanafunzi ambao hawatapata mkopo, nitashangaa” amesema Magufuli.
Rais Magufuli alitoa kauli hiyo kama mfano kwa viongozi aliowateua kutatua matatizo ya wananchi wao kwa wakati.
chanzo:Mwananchi.
Comments