Katibu
Mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji anayeshughulikia
maendeleo ya viwanda, Dk Adelhelm Meru amestaafu utumishi wa umma huku
akiwataka watumishi wa wizara hiyo wasameheane.
“Kwa
kipindi tulichokuwa pamoja kuna mengi tuliyakamilisha. Naomba
tusameheane tulipokosana kwa sababu hakuna mkamilifu,” alisema Dk Meru
ambaye anatarajia kujielekeza kwenye ujasiriamali muda mfupi ujao.
Dk
Meru aliteuliwa na Rais John Magufuli kushika nafasi hiyo Desemba 2015
kabla hajastaafu wiki iliyopita kuhitimisha miaka 37 ya utumishi wake.
Licha
ya wizara hiyo yenye makatibu wakuu wawili ambayo sasa itabakiwa na
mmoja, Wizara ya Nishati na Madini imebakiwa na naibu baada ya aliyekuwa
katibu mkuu wake, Profesa Justin Ntalikwa kutumbuliwa mwishoni mwa
Machi na nafasi yake kubaki wazi mpaka sasa.
Akizungumza
kwenye hafla ya kumuaga, Waziri wa Viwanda na Biashara, Charles Mwijage
alimpongeza kwa kumaliza salama utumishi wa umma na kumsifu kwa umahiri
wake katika kutekeleza sera ya maendeleo ya viwanda. “Ulikuwa mstari wa
mbele kubuni mbinu na mikakati ya kuharakisha ujenzi wa viwanda
nchini,” alisema Mwijage.
Dk
Meru aliwashukuru wafanyakazi wa wizara hiyo kwa ushirikiano waliompa
na kuwaomba waendelee nao kwa watendaji wengine katika kuijenga Tanzania
ya viwanda.
Kustaafu
kwa Dk Meru ambaye alikuwa mkurugenzi mkuu wa kwanza Mamlaka ya Ukanda
Maalumu wa Uwekezaji (EPZA) kunaongeza nafasi za watendaji ambao Rais
Magufuli anapaswa kuzijaza. Nafasi nyingine zilizo wazi kwa sasa ni ile
ya waziri na katibu mkuu wa nishati na madini.
chanzo:Mpekuziblog.
Comments