
Kikao hicho kimefanyika jijini Dar es Salaam majira ya asubuhi na imeelezwa kuwa miongoni mwa walihudhuriwa ni pamoja na Spika wa bunge Job Ndugai, Naibu Spika, Dk Tulia Ackson, Katibu wa Bunge, Thomas Kashilila, Mbunge wa Vunjo, James Mbatia, Mbunge wa Hanang’, Dk Mary Nagu na ndugu watatu wa Lissu, wanaume wawili na mwanamke mmoja.
Mbunge wa Vunjo james Mbatia, amekiri kufanyika kwa kikao hicho ingawa hakuwa tayari kusema chochote kuhusiana na kikao na kuelekeza kuwa aulizwe Spika Ndugai.
“Ni kweli tulikuwa kwenye kikao na familia ya Lissu, lakini siwezi kusema tumezungumzia nini. Kwa taarifa zaidi nendeni kwa Spika au Katibu wa Bunge, walikuwepo pia ndugu zake watatu, wafuateni wanaweza kuwaeleza,” alisema Mbatia.
Msemaji wa familia ya Lissu, Alute Mughwai alisema kikao hicho kimefanyika kati ya familia na uongozi wa Bunge kuhusu mambo yanayomhusu Lissu lakini bado hakijakamilika, kimeahirishwa baada ya Chadema kupitia kwa mwenyekiti wake Freeman Mbowe kupewa mwaliko lakini hawakuweza kufika.
“Siwezi kukwambia tumezungumzia nini, moja ya masharti tuliyopeana ni kutokusema hadharani mambo tuliyoyajadili lakini yanamuhusu Lissu. Wote ‘interest’ yetu ni kuona Lissu anapona na kuendelea na majukumu yake kama kawaida,” alisema Mughwai.
Nae mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano, Uenenezi na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema alipoulizwa kuhusu kikao hicho amesema taarifa kuhusu kikao hicho zilipelekwa Ofisi ya Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni na siyo kwenye chama.
chanzo: zanzibar24.
Comments