Chama
cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Singida kimesema sababu zilizotolewa na
aliyekuwa Mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu za kuacha ubunge
hazina mashiko, isipokuwa kilichomsukuma kufukia uamuzi huo ni hasira za
kukosa uwaziri.
Katibu
wa CCM mkoani Singida, Jamson Mhagama alisema jana Jumatatu Oktoba
30,2017 kuwa, “Kwa maono yake ameona siasa za nchi haziendi vizuri na
kuamua kwenda kusaka siasa zitakazompendeza, tunamtakia kila la kheri.
Ila tunamwonya kuwa asitarajie tena kupata ubunge kupitia Chadema
anakolilia kwenda, CCM itashinda kwa kishindo katika uchaguzi mdogo
ujao,” alisema.
“Wananchi
walimwamini Nyalandu katika vipindi vyote vinne kwa kumpa kura za
kutosha za nafasi ya ubunge. Kupitia kura hizo, Nyalandu amesifika na
kujulikana kila kona sasa ameamua kuwapa kisogo wakazi wa jimbo la
Singida Kaskazini, jina lake linaenda kufutika na hatasikika tena,”
amesema Mhagama.
Katika
hilo, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Singida, William Mwang’imba amesema
kwa jumla wilaya haina shida na Nyalandu na kwa kuwa ameamua kuondoka,
basi aende salama.
Tofauti
na kauli hizo za CCM, Chadema Mkoa wa Singida imempongeza Nyalandu kwa
uamuzi wake, ikisema milango ipo wazi kwa yeye kujiunga na chama hicho.
Mwenyekiti
wa Chadema mkoani Singida, Shaban Limu amesema kwa mujibu wa katiba ya
chama hicho, wanapokea mtu yeyote kutoka kokote kuwa mwanachama.
“Alichofanya
Nyalandu ni sahihi. Wapo baadhi ya viongozi wakiwemo mawaziri na
wabunge hawaridhishwi na hali iliyopo sasa lakini ni waoga, wanaogopa
kupoteza masilahi yao,” amesema.
chanzo:Mpekuziblog.
Comments