Mkazi
wa Chato mkoani Geita, Obadia Kiko (41), amefikishwa katika Mahakama ya
Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na shtaka la kusambaza taarifa za uongo
kupitia mtandao wa kijamii wa Facebook kuhusu mazungumzo kati ya
Serikali na wawakilishi wa kampuni ya Acacia.
Wakili
wa Serikali, Leonard Challo amedai mahakamani kuwa Agosti 3, 2017 huko
Chato Geita mshtakiwa huyo alifanya kosa hilo kupitia mtandao huo wa
kijamii wa Facebook.
Challo
ametoa madai hayo leo Jumanne mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard
Mashauri. Mshtakiwa huyo anadaiwa kusambaza maneno kuwa "Taarifa kutoka
kikao cha mazungumzo kati ya Serikali na wawakilishi wa kampuni ya
Acacia kuwa wanasheria wa upande wetu wanashindwa kutafsiri baadhi ya
vifungu vya sheria hadi kufikia kuomba msaada kwa wanasheria wa Acacia
sasa huoni hivi ni vituko mwizi anakusaidia sheria haahaa haha."
Inadaiwa
aliendelea kusambaza maneno kuwa, "mazungumzo bado yanaendelea lakini
wanasheria wetu wamebanwa sana ukizingatia wale jamaa wana vielelezo
vyote vya mikataba kiukweli tumuombe Mungu maana Serikali ikitaka
kuvunja mkataba na Acacia gharama kubwa zitatuusu."
"Lakini
pia kuendeleza uvyama utatugharimu saana, baada ya mh. Rais Magufuli
angewashirikisha mawakili wasomi waliokwishaiva wakili Lissu, wakili
Kibatara na Fatma Karume kwenye mambo ya umuhimu kama haya yeye kaleta
uchama sasa itatugharimu .// Dicteta Magufuli mist go" . Maneno hayo
yanadaiwa kusambazwa na mshtakiwa huyo kupitia mtandao huo wa kijamii wa
Facebook.
Wakili Challo amedai kuwa maneno hayo yalikuwa na lengo la kupotosha umma.
Baada ya kusomewa shtaka hilo, mshtakiwa huyo alikana na upande wa mashtaka ukadai kuwa upelelezi bado haujakamilika.
Kwa upande wa Wakili Peter Kibatala anayemtetea mshtakiwa huyo aliomba mteja wake apatiwe dhamana na kwa masharti nafuu.
Wakili Challo alieleza kuwa hana pingamizi la dhamana.
Hakimu Mashauri alimtaka mshtakiwa huyo kuwa na wadhamini wawili wanaoamika ambao kila mmoja atasaini bondi ya Sh 5 milioni.
Kesi imeahirishwa hadi Oktoba 16, 2017. Hata hivyo mshtakiwa huyo hakuwa na wadhamini.
chanzo:Mpekuziblog.
Comments