Wenye magari ya mchanga yaliyokamatwa kitanzini.

Idara ya Misitu na Maliasili Zisizorejesheka, imesema hakuna njia mbadala kwa wamiliki wa magari yaliyokamtwa na shehena ya mchanga ukiwa unasafirishwa bila kibali, ni kulipa faini halali au kushitakiwa mahakamani.

Jana uongozi wa idara hiyo uliwaita wamiliki wa magari hayo na uongozi wa jumuiya ya madereva na wenye magari ya mchanga ofisini kwake Maruhubi kwa ajili ya kujadiliana jinsi ya kumaliza kadhia hiyo nje ya mahakama.


Takriban magari 50 ya uzito wa tani tafauti  yalikamatwa kati ya Julai 4 na 5 mwaka huu katika kijiji cha Donge Wilaya ya Kaskazini ‘B’ yakiwa na shehena za mchanga unaodaiwa kuwa ulikuwa ukisafirishwa bila kibali jambo ambalo ni kosa kwa mujibu wa sharia namba 2 ya mwaka 2015.

Aidha baadhi ya madereva wa magari hayo wamedaiwa kuonesha risiti bandia kutaka kuhalalisha uchimbaji na usambazaji wa rasilimali hiyo waliyokamatwa nayo.

Akizungumza katika mkutano huo, Msaidizi Ofisa Mkuu anayeshughulikia programu katika Idara ya Misitu na Maliasili Zisizorejesheka Makame Kitwana Makame, alisema magari manne kati ya hayo, teari yameshafunguliwa kesi mahakamani.

Alieleza kuwa kosa walilolifanya ni miongoni mwa makosa ya uhujumu uchumi na limo mikononi mwa Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar (ZAECA).na uzito wa mchanga uliokamatwa ni tani 5,340, ambao kama ungelipiwa malipo halali tangu shimoni, idara ingeingiza shilingi 38,495,400.

“Ni juu ya wenye magari kuamua. Kwa walio tayari kulipa wajaze fomu maalumu tutakazowapa ili wamuombe Mkurugenzi wa Mazingira ambaye kisheria ndiye mwenye mamlaka, na wasiotaka tuwapeleke mahakamani ambako pengine wakikutwa na hatia ama watatozwa faini au pamoja na kifungo,” alifafanua ofisa huyo.

“Magari haya manne yaliyofikishwa mahakamani ndiyo yenye kesi ya msingi ya risiti za kughushi na hayo mengine yaliyobeba mchanga bila kibali halali kadhia yao inasimamiwa na Idara ya Misitu,” alifahamisha Ofisa Dhamana wa Uchunguzi  ZAECA Makame Khamis Hassan, .

Kwa upande wake, Mwanasheria kutoka Mamlaka ya Mazingira aliyekuwepo kwenye mkutano huo Saada Mussa Said, alisema kwa mujibu wa kanuni, watu wanaochimba mchanga hawatakiwi kuchimba zaidi ya mita tatu, lakini akasema wengi wao wanapuuza sharti hilo na hivyo kuikaribisha Zanzibar katika janga la kimazingira.

Alisema taratibu zinaelekeza kuwa mashimo yanayochimbwa mchanga lazima baadae yafukiwe ili kuipa nafasi ardhi kutumika kwa shughuli nyengine, jambo alilosema kama halikufanyika, athari yake itakuwa kubwa kwa jamii yote.

Alitoa wito kwa wananchi kutunza mazingira, akisema wajibu huo si wa idara au mamlaka za serikali pekee bali ni wa wananchi wote kwani linapotokea janga kila mmoja ataathirika kwa namna moja au nyengine.

Mwenyekiti wa jumuiya ya madereva na wamiliki wa magari ya mchanga Abbas Ussi Haji, alisema zaidi ya miezi miwili sasa tangu kukamatwa kwa magari hayo, mamlaka ilipaswa kuzipeleka mahakamani mara moja kama zilikuwa na makosa.

“Kuzuiliwa magari yetu kwa muda wote huo ni kutusababishia usumbufu. Lakini mtu hawezi kutoka shimoni na mchanga bila kibali na kama kimeonekana ni feki hakukuwa na haja ya kuzuia magari kwa zaidi ya miezi miwili sasa,” alieleza.

Hata hivyo, baadhi ya madereva na wamiliki hao, wamelalamikia magari yao kuandikiwa tani nyingi zaidi ya uhalisia, jambo ambalo uongozi wa Idara ya Misitu umelikanusha ukisema baadhi ya watu hao wameghilibiwa na wenzao waliowauzia risiti za magari mengine.
chanzo: zanzibar24.

Comments