Waziri wa zamani akataa majibu bungeni.

Waziri wa zamani katika Serikali ya Awamu ya Nne, George Mkuchika ameyakataa majibu ya Serikali bungeni akisema yamejaa ghiliba.
Katika swali la nyongeza bungeni leo Ijumaa, Mkuchika amesema majibu ya Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage yanakatisha tamaa kwake na kwa wananchi wa jimbo lake la Newala kwa kuwa yamekuwa ni yaleyale kwa kila mwaka lakini hakuna mabadiliko.

Kwenye swali la msingi mbunge huyo ametaka kujua Serikali ina mpango gani wa kuvifufua na kuviboresha viwanda vikubwa viwili vya kubangua korosho kwa lengo la kuongeza thamani ya zao hilo, kupanua ajira na kukuza uchumi wa viwanda.
Wakati huohuo, Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye ametaka Serikali kutoa majibu ya moja kwa moja ni kwa nini inashindwa kuwanyang’anya viwanda watu walioshindwa kuviendeleza na kuwapa wengine ikiwemo wamiliki wa viwanda vya korosho jimboni kwake.
Akijibu swali hilo, Waziri Mwijage amesema Serikali ilitekeleza sera ya ubinafsishaji na kurekebisha mfumo wa uendeshaji wa mashirika ya umma, vikiwemo viwanda.
Mwijage amesema katika kutekeleza sera hiyo, viwanda 10 vya kubangua korosho nchini vikiwemo viwili vilivyopo wilayani Newala (Newala I na Newala II) vilibinafsishwa.
Amesema mwaka 2005, Serikali iliuza asilimia 100 ya hisa za kiwanda cha Newala I kwa kampuni ya M/s Agro Focus (T) Limited kwa bei ya Sh75 milioni ambayo ililipwa.
“Mwekezaji alifanya uwekezaji mkubwa ambao uliwezesha kufanya uzalishaji mpaka wa mwaka 2013 alipofunga kiwanda,” amesema. Amesema wizara inachofanya ni kuhakikisha viwanda vyote vinafanya kazi.
Waziri amesema kiwanda cha Newala II chenye uwezo wa kubangua tani 3,500 kwa mwaka kilibinafsishwa kwa kampuni ya Micronix Systems Ltd kwa Sh75 milioni mwaka 2004 na mwekezaji alifanya ukarabati wa kuongeza mashine mpya, vyumba vya kukaushia korosho na jenereta ya kuendesha kiwanda.
“Kutokana na ukarabati huo unaoendelea, ubanguaji wa korosho umekuwa ukiongezeka mwaka hadi mwaka na takwimu zinaonyesha kuwa, mwaka 2013 walibangua tani 1,500.
Amesema mwaka 2014 tani 1,800 zilibanguliwa na mwaka 2016 walibangua tani 3,000.
chanzo:Mwananchi.

Comments