Waziri wa Elimu Zanzibar awataka wanafunzi wa kike kujikita katika masomo ya Sayansi.

WAZIRI wa Elimu Mafunzo na Amali Riziki Pembe Juma amewasisitiza wanafunzi  wa kike  kujikita zaidi kusoma  masomo ya  sayansi kwani  ndiyo yenye  fursa kubwa za ajira  hivi sasa.

Akizungumza na wanafunzi wa skuli zilizoshiriki mashindano ya masomo ya Sayansi kwenye fainali iliyozikutanisha  Skuli ya Mikindani na Fidel Castro katika Ukumbi wa Kariakoo, Waziri Riziki alisema   masomo ya sayansi  yana umuhimu mkubwa katika karne ya sasa ya Sayansi na Teknolojia.


Amesema kutokana na umuhimu huo Jumuiya ya kuhamasisha watoto wa kike kusoma masomo ya Sayansi  (FAWE) inachukua  juhudi ya kuwashajihisha  kuyapenda  masomo hayo.

Alisema hivi sasa Tanzania inaelekea katika uchumi wa viwanda na wataalamu  wa sayansi katika fani mbali mbali watahitaji hivyo upo umuhimu mkubwa kwa wanafunzi wa kike  kujikita katika masomo ya Sayansi na Teknolojia.

“Tunahitaji wataalamu wa kike  kwenye uvumbuzi wa mafuta na gesi, walimu wa kufundisha masomo ya  Sayansi, mafundi mitambo wa viwandani, lazima mufuzu katika masomo ya sayansi,”alisisitiza Waziri wa Elimu.

Allishukuru Jumuiya ya FAWE kwa jitihada  wanazochukuwa kwa kuwahamasisha watoto wa kike kusoma masomo haya wakielewa kwamba  unapomuelimisha mtoto wa kike ni sawa na  kuielimisha jamii.

Waziri wa Elimu aliwapongeza wanafunzi wa skuli ya Fidel Cstro Pemba na Mikindani ya Unguja kwa kuingia fainali katika mashindano hayo yaliyoshirikisha skuli kumi za Unguja na Pemba.

Aliahidi Wizara yake  itaongeza mashirikiano na FAWE  ili iweze kuleta mabadiliko makubwa zaidi  kwa wanafunzi wa kike  na wanawake walioko katika mazingira magumu ambapo ndio lengo kuu  la Jumuiya hiyo.

Waziri Riziki aliwashukuru Milele Foundation kwa kuzifadhili skuli zote 10 zilizoshiriki  mashindano hayo  na kusaidia ujenzi wa  madarasa skuli mbali mbali.

Mratibu wa Jumuiya ya FAWE Hinda  Abdullah Ajmy  alisema wameweka mikakati ya kuandaa  mashindano ya aina hiyo kwa lengo la kuongeza  nguvu  katika kuibua vipa kwenye  masomo ya sayansi.

Afisa mipango wa mradi wa Mradi wa Masomo ya Sayansi, Teknolojia, Ufundi na Hesabati (STEM) Warda  Mustafa Hamid  alisema lengo la mradi huo ni kuhamasisha  wanafunzi waweze kusoma  sayansi na kuwajengea uwezo kuhamasisha wenzao .

Katika fainali hiyo skuli ya Fidel Castro ya Pemba imeshika nafasi ya kwanza kwa kupata alama 55 na Skuli ya Mikindani Unguja imepata alama 48.07 na kushika nafasi ya pili.

chanzo:Zanzibar24

Comments