
Walisema kazi wanayoifanya ambayo ndio azma ya serikali ya kuwasaidia
wananchi katika kutambua haki na wajibu wao, ni nzuri ingawa bado
sheria za nchi haziwatambui rasmi, hivyo wakati sasa umefika.
Wakizungumza na mwandishi wa Zanzibar24 walisema kwa vile kazi hiyo
imekuwa ikiwasaidia wananchi kupata haki zao, lazima mihimili ya nchi
iwatambue rasmi.
Kamanda wa Polisi mkoa wa kusini Pemba, Sheikhan Mohamed Sheihan
alisema kabla ya kuwepo kwa wasaidizi wa sheria, ilikuwa wananchi hawana
uwelewa wa kuwasilisha mashauri yao, kituoni hapo.
Alisema ingawa kwa sasa hali tofauti, maana wapo wananchi wakati
mwengine wanaowaelimisha Polisi, juu ya taratibu na haki zao wanapokuwa
kituoni hapo.
“Mimi nasema hawa wasaidizi wa sheria, lazima sasa kuwe
na sheria maaluma inayowatambua, maana kazi wanayoifanya ndio ile ile
inayofanywa na vyombo vyengine, sasa kusiwe na sababu ya kutotambulika
rasmi”,alisema.
Nae Sheha wa shehia ya Mtemani Jimbo la Wete, Mrisho Juma Mtwana ‘magogo’ alisema lazima kwa serikali kuandaa sheria ya haraka, ili kuwatambua wasaidizi wa sheria, waliopo majimboni.
“Sasa hata sisi masheha wakati mwengine huwa wanatueleza
taratibu na kazi zetu hawa wasaidizi wa sheria, maana wao wamepata
uwelewa wa sheria, sasa ni jambo jema, wakatambulika rasmi”,alishauri.
Msaidizi wa sheria wa Jimbo la Chakechake Riziki Hamad Ali, alisema
kama zipo taasisi zimeshatengenezewa sheria hakuna sababu na wao
wasitambuliwe na sheria.
“Mimi naamini kama tukitambulika rasmi na sheria, hata
vile vyeti vya uhitimu tunavyopewa, vinaweza kutusaidia katika kupata
ajira, maana tunakuwa na uwelewa wa sheria.
“Mwanafunzi wa skuli anatambuliwa na sheria, karafuu zina
sheria yake, Ukimwi unasheria yake, magazeti, barabara, waajiriwa
serikali, hivyo ni vyema na sisi wasaidizi wa sheria, tukatengenezewa
sheria yetu”,alieleza.
Kwa upande wake Katibu tawala wilaya ya Micheweni Hassan Abdalla
Rashid, alisema iwapo wasaidizi wa sheria watatambuliwa na sheria za
nchi, itakuwa ni jambo jema maana sasa watakuwa wanafanyakazi zao kwa
upana.
Hata hivyo alisema, tayari binafsi ameshawahi kushiriki katika vikao
vya awali vinavyoonyesha kuwa, sheria ya kuwatambua wasaidizi wa sheria
inakuja.
“Ijapokuwa wanavitambulisho vya kazi zao, lakini haitoshi
lazima na sheria za nchi ziwatambue, ili wawe na mapana ya kazi yao,
tena popote pale”,alifafanua.
Mratibu wa Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar ZLSC taswi la Pemba
Fatma Khamis Hemed, alisema umuhimu wa wasaidizi kutambuliwa upo, moja
ikiwa ni kufanya kazi zai zao bila ya wasiwasi.
“Kitu kinapokuwa kinatambuliwa na sheria za nchi, basi
ndio kipo kisheria, lakini kinyume chake ndio hakitambuliwa kisheria,
hivyo lazima serikali ipeleke msaada wa sheria hiyo”,alifafanua.
Afisa Upelelezi wa Dawati la jinsia na watoto kutoka jeshi la Polisi
Mkoa wa kusini Pemba, Hamad Fakih Ali, alisema wasaidizi wa sheria,
wamekuwa wakiwasaidia katika mapambano dhidi ya kesi za udhalilishaji.
“Sisi wamekuwa wakituibuliwa hata kesi za udhalilishaji,
maan kama Jeshi la Polisi, hatupo kila pahala, lakini kuanzishwa kwa
mpango wa wasaidizi wa sheria, sasa afadhali twashirikiana vyema”,alifafanua.
Omar Juma Ameir mkaazi wa shehia ya Sizini alisema, yeye alifanikiwa
kurejeshewa fedha zake shilingi zaidi ya 1,000,000 (milioni moja),
alizotapeliwa baada ya kuuziwa kiwanja kilichokwisha uzwa.
“Mimi nilimtumia msaidizi wa sheria wa Jimbo la Winwgi,
na sikwenda Polisi, maana ningechukuwa muda mrefu, lakini alipoitwa tu
na msaidizi wa sheria huyo alienitapeli, alikubali kunilipa mara mbili,
bila ya mashaka”,alifafanua.
Mratibu wa wasaidiz wa Sheria Pemba, Safia Saleh Sultan alisema
wasaidiz hao wa sheria, husoma kwa muda wa miaka miwili mambo mbali
mbali, ikiwa ni pamoja na sheria ya ushahidi, mfumo wa sheria wa Afrika
wa Mashairiki, Katiba na mfumo sheria, Sheria ya mikataba, sheria ya
jinai, sheria ya madhara, sheria ya madai na sheria ya utawala.
Mradi wa wasaidizi wa sheria ambao upo chini ya Kituo cha Huduma za
Sheri Zanzibar ZLSC, kwa kisiwani Pemba pekee tayari wapo wasaidizi wa
sheria 96 ambao wameshahitimu na wapo kila Jimbo la uchaguzi.
chanzo: zanzibar24.
Comments