Kila mwezi, Serikali inatumia zaidi ya Sh18 bilioni kugharamia utekelezaji wa sera ya elimu bure ya msingi kuanzia darasa la awali hadi kidato cha nne.
Hata hivyo, utekelezaji wa sera hiyo unaolenga kutoa fursa ya elimu kwa watoto wote nchini bila kujali uwezo wa kiuchumi wa wazazi au walezi wao, unakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwamo tatizo la mimba za utotoni kwa wanafunzi.
Serikali na wadau wa elimu wanafanya jitihada kukabiliana na tatizo hilo, kama ambavyo hivi karibuni Shirika la Kivulini Mwanza lilivyoandaa midahalo iliyoshirikisha wanafunzi zaidi ya 3,243 wa shule za msingi na sekondari jijini humo kujadili suala hilo.
Midahalo hiyo iliyokuwa na kauli mbiu ya “Madhara ya mimba za utotoni nani alaumiwe?, ilishirikisha wanafunzi kutoka shule za msingi za Sweya, Igombe, Bugogwa, Kisundu na Kayenze, huku washiriki kutoka sekondari wakitoka Bugogwa, Sangabuye na Luchelele.
Walimu, maofisa wa jeshi la polisi kutoka Dawati la Jinsia na Watoto, wataalamu wa afya, watendaji wa kata na mitaa na waandishi wa habari pia walikuwapo kudadavua namna ugumu wa maisha na shughuli za kiuchumi zinavyochangia mimba za utotoni kwa wanafunzi.
Makundi hatarishi yatajwa
Pamoja na uduni wa maisha kwa familia nyingi, baadhi ya wanafunzi waliopata fursa ya kuchangia mada katika midahalo hiyo iliyofanyika kwa wiki mbili mfululizo, wametaja makundi kadhaa ya kijamii wanayodai ni adui wa maendeleo ya kielimu kwa watoto wa kike.
Waendesha bodaboda, wafanyabiashara wa chips, vinyozi, wavuvi na wa urembo ni miongoni mwa makundi ya kijamii yanayotajwa kuongoza kwa kuwarubuni wanafunzi na kuingia nao kwenye uhusiano wa kimapenzi na hatimaye kuwapa ujauzito.
“Wandesha bodaboda wao huwarubuni wanafunzi kwa kuwapa lifti, huku wale wauza chips maeneo ya karibu na shule hutumia ofa ya chakula kuwanasa wanafunzi wanaotoka familia duni kimaisha wasiomudu gharama za kununua chakula kila siku wawapo shuleni,” anasema Kabula Makoye, Mwanafunzi wa kidato cha pili katika Shule ya Sekondari Sangabuye.
Pia, Makoye anataja adui wengine kwa wanafunzi kuwa ni vibanda vya kuonesha mikanda ya video mitaani maarufu kama vibanda umiza.
Mwanafunzi kutoka Shule ya Msingi Sweya, Tausi Yusuph ametaja matukio ya ubakaji hasa kwa wanafunzi wanaotemmbea umbali mrefu kwenda na kurudi shuleni kuwa ni miongoni mwa adui wa elimu.
“Wapo wanafunzi wanaotembea umbali wa zaidi ya kilomita kumi kwenda na kurudi shuleni kila siku; hawa wanaangukia kwenye mtego wa waendesha bodaboda wanaowashawishi kwa lifti,” anasema mwanafunzi huyo.
Pia, ametaja mila na desturi, ulaghai wa walimu kupitia masomo ya ziada na tabia ya baadhi ya wazazi kuwageuza kitega uchumi watoto wao hivyo kuchangia mimba za utotoni.
“Baadhi ya wazazi wanaoishi mwambao wa Ziwa Victoria huwatumia watoto wao wa kike kama chambo kupata kitoweo kutoka kwa wavuvi; unakuta mzazi anampa binti yake Sh1,000 kwenda mwaloni kununua samaki wa kutosha familia,” anasema Leticia Sawali, mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Bugogwa.
Leticia anasema katika mazingira hayo, mtoto wa kike hulazimika kujilengesha au kujirahisisha kwa wavuvi ili kupata samaki wengi kwa fedha kidogo na mwishoni huishia kupata si tu ujauzito, bali pia hatari ya kuambukizwa magonjwa ya zinaa.
Madhara ya ngono umri mdogo
Kwa mujibu wa mtaalamu wa afya kutoka katika Kituo cha Afya cha Karume kilichopo Kata ya Bugogwa, Dk Gasper Lugela pamoja na ujauzito, wanafunzi wanaopata mimba katika umri mdogo pia wanakabiliwa na hatari ya kupoteza maisha wakati wa kujifungua kutokana na viungo vyao vya uzazi, hasa nyonga kuwa ndogo.
“Wengi wao hutokwa na damu nyingi wakati wa kujifungua kutokana na kuchanika sana,” anasema mtaalam huyo.
Anataja madhara mengine kiafya kuwa ni kupata kifafa cha mimba, kuharibika kisaikolojia na magonjwa ya kuambukiza ukiwamo Ukimwi, kisonono na kaswende kutokana na uelewa mdogo kuhusu njia za kujikinga.
Dk Lugela anasema licha ya kuwa kwenye hatari ya kupata tatizo la fistula, mimba katika umri mdogo pia, huongeza uwezekano wa mhusika kujifungua mtoto njiti au mwenye mtindio wa ubongo.
Kuhusu tatizo la kisaikolojia, mtaalamu mwingine kutoka Kituo cha Afya cha Sweya, Dk Matrida Kahondo anasema anayekatisha masomo kwa ujauzito hupata madhara kisaikolojia kila anaposhuhudia wenzake wakiendelea na masomo na kufanikiwa kimaisha, huku yeye akiishi maisha duni baada ya kuacha shule.
“Wanaopata ujauzito hupoteza ndoto zao kimaisha; hawawezi kufikia malengo ya kuwa walimu, madaktari, askari, wanasheria na taaluma na hii huwaathiri kisaikolojia,” anasema Dk Kahondo.
Mabazazi waepa sheria
Kwa mujibu wa Sheria ya Mimba za Utotoni namba 29 ya Mwaka 2009, mtu anayethibitika kumpa mimba mwanafunzi au mtoto mwenye chini ya miaka 18 anastahili adhabu ya kifungo cha miaka 30 jela.
Lakini, wengi wanaowapa mimba wanafunzi hukwepa adhabu hiyo kwa kula njama na wanafunzi wenyewe, wazazi au wenye dhamana ya kusimamia utekelezaji wa sheria hiyo.
“Baadhi ya wazazi hawaripoti matukio ya watoto wao kupewa mimba. Hata wale wanaoripoti hawafiki mahakamani kutoa ushahidi kesi zinapofunguliwa,” anasema Said Mandi, askari polisi anayesimamia Dawati la Jinsia na Watoto kutoka Kituo cha Polisi Bugogwa na Igombe.
Anasema hiyo husababishwa kitendo cha baadhi ya wazazi kupokea mahari au ‘faini’ kutoka kwa watuhumiwa kama kifunga mdomo.
Hata hivyo, Fortunata Scanda polisi anayehudumia Kituo cha kushughulikia kesi za ukatili wa kijinsia katika Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Mwanza, Sekou-Toureni, anasema kufunguliwa kwa kituo hicho kumerahisisha upatikanaji wa takwimu za matukio hayo.
Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto Mkoa wa Mwanza, Bethninsimbo Shija anasema urahisi wa kufikia huduma kupitia kituo hicho, umepunguza matukio ya ukatili wa kijinsia kutoka 662 kati ya Januari hadi Juni 2016, hadi matukio 558 kwa kipindi kama hicho mwaka huu.
Mtendaji wa Kata ya Sangabuye, Juma Ngoloma anasema katika kata yake elimu kwa umma imesaidia kupunguza matukio ya mimba kwa wanafunzi kutoka saba kati ya Januari hadi Juni mwaka jana, hadi kufikia matukio matatu yaliyoripotiwa kwa kipindi hicho mwaka huu.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kayenze, Mayenga Mbalala anaiomba Serikali na wadau kuongeza kasi ya utoaji wa elimu kwa umma kama njia ya kukabiliana na tatizo la mimba za utotoni kwa wanafunzi.
Mkazi wa Mtaa wa Kayenze, Cherles Makungu aliyepata fursa ya kushiriki moja ya midahalo anataja tabia ya baadhi ya wazazi kutozungumza masuala ya afya ya uzazi na watoto wao kuwa inachangia mimba za utoto.
Mtaalamu wa masuala ya Jinsia Kivulini, Grace Mussa anasema mradi wa kupiga vita mimba za utoto unaofadhiliwa na The Foundation for the Civili Society, umebaini kuwa siyo watoto pekee, bali hata wazazi hawana elimu ya afya ya uzazi.
Anasema baadhi wa wazazi pia huchukulia suala la afya ya uzazi kama aibu isiyofaa kuzungumzwa kati ya mzazi na mtoto.
chanzo:Mwananchi.
Comments