Wadau wa maendeleo wamekabidhi Sh227.76 bilioni kwa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa ajili ya miradi ya sekta ya afya.
Fedha hizo za mfuko wa pamoja zimekabidhiwa leo Jumatatu na Balozi wa Denmark nchini, Einar Jensen kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Doto James na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dk Mpoki Ulisubisya.
Akizungumza baada ya makabidhiano yaliyofanyika Hazina, Dk Ulisubisya amesema mfuko huo ulioanzishwa mwaka 1999 unalenga kuongeza nguvu za Serikali katika kupeleka mahitaji ya afya kwa wananchi.
Amesema fedha hizo hupokewa na Wizara ya Fedha na kupelekwa Wizara ya Afya na ya Tamisemi.
Dk Ulisubisya amesema asilimia 80 ya fedha hupelekwa moja kwa moja kwenye maeneo yanayotoa huduma za afya kwa wananchi katika halmashauri na vituo vya kutolea huduma.
Amesema asilimia 20 inayobaki ni kwa ajili ya shughuli za utawala na ufuatiliaji wa makubaliano ya madhumuni ya fedha hizo.
“Mwaka huu tumekubaliana fedha zinakwenda kuangalia huduma za afya kwa ajili ya mama na mtoto, uzazi pingamizi na huduma za chanjo kwa sababu ni afua muhimu kuzuia maradhi, pia kupunguza vifo vya akina mama,” amesema.
Balozi wa Denmark nchini, Jensen amesema wataendelea kuiunga mkono Serikali kwa fedha za wadau wa maendeleo.
chanzo:Mwananchi.
Comments