Tusisubiri kusukumwa na Rais kwa dhamana tulizokubali kuzibeba.

Siku kadhaa zilizopita, baadhi ya vyombo vya habari viliukariri uongozi wa Halmashauri ya Wilaya  ya Kaskazini ‘A’ ukisema kuwa tayari umeanza kutekeleza agizo lililotolewa na Mhe. Rais Dk. Ali Mohamed Shein, kutaka kuondolewa kwa majaa yaliyokithiri katika kijiji cha Nungwi.

Uongozi huo ukasema umefanya utafiti mdogo na kubaini chanzo cha kuibuka majaa hayo na kuzagaa ovyo kwa uchafu kila kona ya kijiji hicho kilichoko kwenye ukanda wa utalii.


Rais alitoa agizo hilo katika hutuba yake ya majumuisho kufuatia ziara ya kikazi aliyoifanya Mkoa wa Kaskazini Unguja, ikiwa miongoni mwa ziara zake za mikoa yote ya Zanzibar.

Lakini licha ya agizo la kiongozi wa juu wa nchi, bado kijiji hicho kinasikitisha kutokana na  taka nyingi zinazochafua mandhari ya eneo hilo ambalo sasa ni miongoni mwa vivutio vikubwa vya utalii nchini.

Uchunguzi umebaini kwamba kiwango kikubwa cha taka zinazozagaa kwenye majaa na ufukwe wa Nungwi, ni mifuko meusi ya plastiki iliyopigwa marufuku hapa Zanzibar.

Mifuko hiyo hupatikana katika maduka, ikitumika kutilia bidhaa zinazonunuliwa na wateja mbalimbali ambao hatimaye huitupa popote bila kujali kuwa kufanya hivyo kunachafua mazingira na kuitia nchi aibu machoni mwa watalii wanaotembelea ukanda huo.

Kiona mbali kimefurahishwa na hatua zinazochukuliwa sasa na uongozi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo katika kuhakikisha mazingira na maeneo yake yanakuwa safi.

Lakini haikufurahishwa na kitendo cha kutokuona wajibu huo mpaka pale Mhe. Rais alipoiona hali hiyo na kuweka wazi namna alivyokerwa na hivyo kuuagiza uongozi wa halmashauri kulishughulikia tatizo hilo.

Katika hali ya kawaida, na kwa viongozi wanaojali majukumu yao, Nungwi haikupaswa kufikia kiwango hicho cha uchafu kwani mji huo sasa umekua kiuchumi na kibiashara na una vyanzo vingi vya mapato.

Kwa hivyo, sidhani kuwa ukosefu wa fedha unaweza kutajwa kuwa ni sababu ya kushindwa kusimamia suala la usafi kijijini hapo, kwani kama ni vifaa vinaweza kupatikana kwa kiwango cha kutosha.

Katika dhana ya uwajibikaji uliotukuka, haiingii akilini kwamba uchafu na majaa hayo yangesubiri ujio wa mkubwa wa nchi kuyatolea agizo ili yasafishwe.

Je, ingekuwaje kama kiongozi huyo hakuwa na ratiba ya kuzunguka mikoani kwa sasa na miezi kadhaa mbele? Ndio kusema viambo hivyo vingeliendelea kunuka uvundo utokanao na taka majaani zikiwemo za masalia ya samaki ikizingatiwa eneo hilo lipo karibu na soko?

Ikumbukwe kuwa hali hiyo si ya leo wala jana, bali ni ya siku nyingi, hivyo inasikitisha kwamba pamoja na mamia ya macho yanayoona hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa hadi Mhe. Rais alipofanya ziara kijijini hapo.

Ifahamike kuwa halmashauri zina viongozi na watendaji wengi zikiwemo kamati za mazingira, na hizi ni miongoni mwa kazi zao ambazo hazihitaji kusubiri kumurikwa na ‘Kiona mbali’ au agizo la mkubwa pale anapofanya ziara za kikazi.

Uwajibikaji (Accountability) bila kusukumwa kwa amri na maagizo ya viongozi wa juu ndio unaoonesha taswira ya aina ya kiongozi aliyepewa dhamana ya kusimamia mambo kwenye eneo fulani.

Kushindwa kusimamia majukumu ambayo kwayo mtu analipwa kwa ajili ya kuyetekeleza, kunawapa mwanya watu wengine wanaozitamani nafasi hizo kulalamika pembeni na kumteta vibaya.

Na katika hali kama hii, iwapo mtu ataondoshwa kwenye wadhifa alionao, wa kulaumiwa ni yeye mwenyewe na asije kutafuta mchawi.

Kazi ya ‘Kiona mbali’ ni kuonesha njia kwa yeyote anayekengeuka ili ajirekebishe, atekeleze na kusimamia vyema wajibu wake na kutambua kwamba cheo ni dhamana na sio njia ya kuvuta hela bila kutoka jasho.

Chanzo: zanzibar24.

Comments