Polisi
wamelazimika kuwatawanya kwa mabomu ya machozi wafuasi wa vyama vya
Jubilee na muungano wa upinzani wa Nasa baada ya kuzua vurugu katika
ofisi za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (IEBC) zilizoko jengo la Anniversary
Towers.
Wafuasi
wa Nasa waliokuwa wakiimba nyimbo “Chiloba lazima ang’oke” walikabiliwa
na wafuasi wa Jubilee waliokuwa wakiimba “Tunataka amani”. Makundi yote
mawili yalitimua mbio baada ya polisi wa kuzuia ghasia kuwarushia
mabomu ya kutoa machozi.
Huku wakikohoa na wakitafuta mahali salama, wote walikimbia kukwepa kukamatwa.
Maandamano
hayo yamefanyika kuitikia wito uliotolewa jana na kiongozi mkuu wa Nasa
Raila Odinga kwamba wafuasi wake wajitokeze kwa wingi kuandamana hadi
kwenye makao makuu ya IEBC lengo likiwa kumtoa kwa nguvu Ofisa Mtendaji
Mkuu wa IEBC Ezra Chiloba kwa madai ya kuhusika kuvuruga uchaguzi mkuu
uliofanyika Agosti 8.
Maandamano hayo yanafanyika siku chache baada ya Mahakama ya Juu kufuta ushindi wa Rais Uhuru Kenyatta.
Katika
mji wa Kisumu, ambao unatajwa kuwa moja ya ngome za Nasa baadhi ya
wakazi waliandamana hadi ofisi za IEBC na baada ya kufika walitoa wito
maofisa wa ngazi za juu akiwemo Ezra Chiloba wajiuzulu.
Walimshutumu
Chiloba na kikundi chake kwa kufanya njama za kuingilia mchakato wa
uchaguzi mkuu ambao matokeo yaliyompa ushindi Uhuru Kenyatta yalifutwa
na Mahakama ya Juu.
Waandamanao
waliokuwa wamebeba matawi ya miti, mabango huku wakipiga yowe na honi
za pikipiki walianzia barabara ya Obote wakaenda mtaa wa Oginga Odinga
kabla ya kuchukua Barabara Kuu ya Kenyatta na baadaye Mtaa wa Ang’awa
katikati ya jiji.
chanzo:Mpekuzibloog.
Comments