Mwili wa Kamishna mstaafu Zimamoto kuagwa leo.

Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Thobias Andengenye leo ataongoza maofisa na askari kuuaga mwili wa kiongozi mstaafu wa jeshi hilo.
Aliyekuwa Kamishna mstaafu wa Operesheni wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Rogatius Kipali alifariki dunia Septemba 7 akiwa nyumbani kwake Mombasa, Ukonga jijini Dar es Salaam.
Mwili wa Kipali unaagwa leo Jumapili kwa paredi maalumu.

Taarifa ya Kitengo cha Habari na Elimu kwa Umma cha jeshi hilo iliyotolewa jana Jumamosi inasema shughuli za kuaga mwili itafanyika kuanzia saa tatu asubuhi katika viwanja vya Kituo cha Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Ilala, eneo la Faya.
“Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji anapenda kuvitaarifu vyombo vya ulinzi na usalama, maofisa, askari na watumishi wote wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, familia ya marehemu na wale wote walioguswa na msiba huu kwa namna moja au nyingine kujitokeza kwa ajili ya kutoa heshima zao za mwisho,” imesema taarifa hiyo.
chanzo:Mwananchi.

Comments