‘Ukishangaa ya Mussa utayaona ya firauni’ ni msemo uliojidhihirisha baada ya mchimbaji mdogo wa madini Pili Hussein (55) maarufu kama ‘Mjomba Hussein’ kusimulia namna alivyojifanya mwanaume na kuishi mgodini kwa zaidi ya miaka 10 bila kujulikana.
Mwanamke huyo ameeleza kuwa alijulikana baada ya kubambikiwa kesi ya ubakaji iliyoshindwa kuendelea alipoomba akaguliwe mwili wake na kukutwa kuwa kumbe ni mwanamke.
Alisimulia hayo katika viwanja ya Mtandao wa Jinsia (TGNP), lilikofanyika tamasha la 14 la jinsia, mwanamke huyo aliamua kusimulia maisha yake ya kujifanya mwanaume wakati akitaka kutimiza ndoto zake kimaisha kutokana na umaskini.
Pili alisema kilichomsaidia kuishi bila kujulikana ni mavazi yake ya kiume, sauti nzito na umbile la kutokuwa na maziwa kutokana na ukweli kwamba wanawake hawakuruhusiwa kuingia kwenye migodi kufanya kazi hiyo.
Alisema kwa sababu wanawake hawakuruhusiwa kufanya kazi hiyo ya kuchimba madini, njia pekee aliyoitumia kuingia mgodini ni kubadilisha muonekano wake halisi huku akijibatiza jina la Mjomba Hussein ilimradi atimize ndoto zake kimaisha.
“Walikuwa hawataki wanawake, kwa hiyo nilichofanya ni kunyoa zungu, kuvaa makofia makubwa, kaptula na mavazi ya kimasai wakati mwingine,” alisema.
Huku akishangiliwa na wanachama wa TGNP, mwanamke huyo alisema alianza kazi ya uchimbaji madini kama mwanaume halisi.
“Nilikuwa nainua nyundo ya kilo 15, napasua miamba na wakati mwingine nawasaidia wanaume kwa sababu walikuwepo ambao hawakuwa wakiweza kuingia mgodini kwa kamba,”alisema.
Aliendaje
Pili alisema akiwa na umri wa miaka 31 aliamua kwenda mgodini kutafuta kazi huku akijifanya mwanaume.
“Kabla sijaenda mgodini nilikuwa nimeolewa na mwanaume wa kichagga. Kama mnavyojua, niliachwa kijijini mume wangu akaenda kutafuta maisha. Nilipata mtoto mmoja nikaamua kumpeleka kwa wazazi wangu,”alisema.
Pili ambaye hakuwahi kusoma hata darasa la kwanza baada ya baba yake kumpatia kazi ya kuchunga ng’ombe tangu akiwa mdogo, alisema hakuwahi kuonewa wala kuhisiwa kuwa ni mwanaume katika miaka yote aliyoishi kwenye mgodi huo.
“Ilikuwa nikimaliza kazi zangu za uchimbaji wa madini, narudi kwangu maisha yanaendelea. Kuna wakati tulikuwa tunatakiwa kwenda kuoga wote, nilichokuwa nafanya ni kuvaa kaptula na nguo ya juu. Hawakunijua hata kidogo,”alisema.
Alisema maisha yake ya kibabe yaliwafanya wanaume kuwa wanamuogopa na mara zote, aliwatetea wanawake hasa wanaofanya biashara kwenye eneo hilo.
“Walikuwa wananiogopa, sikuwahi kuchezewa na nilishiriki kila kitu wanaume walichofanya,”alisema.
Alisema ili asijulikane alienda kwenye maeneo yanayouzwa pombe na aliwanunulia wenzake bila yeye kunywa.
“Nilikuwa na mirungi kwenye mifuko yangu ya kaptula na mtu akiomba nilimpa. Pamoja na kujifanya hivyo sikuwahi kuonja, kwa sababu kiuhalisia niliigiza tu,”alisema.
Alisema hakusota sana mgodini akabahatika kupata madini ya Tanzanite, yaliyompatia Sh100 milioni.
Mwanamke huyo alisema fedha hizo zilisaidia kutimiza ndoto ya maisha yake kwa kumjengea baba yake nyumba sita.
“Baba yangu anawake sita, hivyo kila mwanamke nilimjengea nyumba nikanunua trekta na hivi nizungumzapo, nimefanikiwa kuwasomesha zaidi ya watoto 30, baadhi yao wapo chuo kikuu,” alisema.
Kusingiziwa kubaka
Kiuhalisia mwanamke huyo aliishi mgodini maisha ya kibabe.
Alisema kuna baadhi ya watu walikuwa wavivu na mara nyingi walikuwa wakimsumbua.
“Siku hiyo nikachukua mayai, nikawapigia kwenye makalio yakapasuka. Kwa sababu walikasirika basi wakanibadilikia na kunisingizia kuwa nimewabaka,”alisema.
Alisema alikamatwa na mgambo, akafikishwa kituo cha polisi ili baada ya uchunguzi kesi hiyo ipelekwe mahakamani.
“Nikiwa polisi niliwaambia wanikague lakini nilitaka mwanamke ndiye afanye kazi hiyo. Polisi walikubali na maajabu yake wakashangaa mimi si mwanaume,”alisema.
Mgodini alioa
Akiwa mgodini Pili alikutana na mwanamke ambaye alikuwa na watoto wadogo akihangaika kupata kazi walau aishi na watoto wake.
“Nilimuhurumia, nikajua kama nikimuacha anaweza kupotea na mwisho watoto wakateseka. Nilimwambia nataka kumuoa, mwanamke yule alikubali nikamjengea nyumba ndogo akaanza kuishi kwangu,”alisema.
Pili hakuwahi kuvua nguo mbele ya mwanamke huyo lakini siku zote alimsisitiza kufanya kazi ya kuuza chakula kwa bidii.
“Ilikuwa akitaka haki ya ndoa namwambia, amekuja kutafuta aachane na masuala hayo. Tuliishi na alinizoea hivyo cha ajabu hakuna mwanaume aliyemgusa kwa sababu wote walijua ni mke wa mjomba Hussein,”alisema.
Hata hivyo baada ya kesi, mwanamke huyo alikuja kugundua kuwa aliishi na mwanamke mwenzake.
“Nilimwambia kama ningemuacha angepotea, sikupenda kuona mwanamke ananyanyasika hata hivyo nilikuwa naogopwa kwa hiyo, yule mama hakunisumbua,”alisema
Mwenyekiti wa wanawake katika Shirikisho la Wachimbaji Wadogo wa Madini, Sara Lusambagora alisema Pili aliweza kwa sababu aliamua kuthubutu.
“Ili kuingia mgodini lazima ujitose na mazingira magumu ya huko yanawafanya wanawake wasiingie kabisa hivyo huyu mwanamke ni mfano kwetu lakini kwa wanawake wote Tanzania,”alisema.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Wachimbaji Wadogo Wanawake wa Madini, Doreen Kissia alisema aligundua Pili ni mwanamke baada ya kubambikiwa kesi ya ubakaji.
“Siku zote nilikuwa najua mwanaume, hili lilitushangaza sana na kwa kweli amekuwa mwanamke wa mfano na ameajiri zaidi ya vijana 70, wanaishi kwa kumtegemea,”alisema.
Mkurugenzi wa TGNP, Lilian Liundi alisema tamasha hilo limelenga kuwafundisha wanawake namna ya kujituma, kutafuta fursa na kuona namna ya kusaidiana hasa kwa wale waliofanikiwa.
Comments