Kama ulidhani kimbunga kilichotokana na ripoti ya uchunguzi wa biashara ya madini ya almasi na Tanzanite kimemalizika kwa vigogo kung’oka, umekosea; bado kuna msururu wa watumizi.
Baada ya kupokea taarifa ya jopo la kutathmini thamani ya madini ya almasi yaliyozuiwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) Alhamisi iliyopita, Waziri wa Fedha na Mipango, Phillip Mpango ameagiza wafanyakazi wote wa Serikali waliohusika kwa njia moja au nyingine kupitisha almasi hiyo, wachukuliwe hatu, ikiwa ni pamoja na kutaifishwa mali zao na kufikishwa mahakamani.
Pia, Serikali imeamua kutaifisha almasi yote ya kampuni ya Williamson Diamonds Limited inayoendesha mgodi wa Mwaduiambayo ilizuiwa JNIA baada ya taarifa kubainisha kuwa wamiliki walidanganya thamani halisi ya madini hayo ya vito.
Ikiwa ni siku mbili baada ya ripoti ya kamati mbili za Bunge kusababisha vigogo wanne kung’oka, watumishi wa Wizara ya Nishati na Madini na taasisi nyingine zinazohusiana na biashara hiyo, wanatarajiwa kufuata mkumbo huo, na tayari baadhi wameshakamatwa wakihojiwa, kwa mujibu wa naibu mkurugenzi wa Takukuru, Brigedia Jenerali John Mbungo.
Mawaziri waliong’oka ni George Simbachawene (Tamisemi) na Edwin Ngonyani (naibu waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano)
Akizungumza JNIA jana alikopokelea taarifa hiyo, Dk Mpango alisema “Tanzania imepigwa vya kutosha hivyo wale wote waliohusika katika upigaji huo washughulikiwe”.
Pia, aliviagiza vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na idara za sheria kuanza kuwachunguza wafanyakazi wa mgodi huo kama walihusika kwa njia yoyote kufanikisha utoroshaji wa rasilimali hizo za Taifa.
Alisema wafanyakazi wote wanaohusika kuanzia uchimbaji wa madini hayo mpaka kule yanakosafirishwa, wamulikwe na vyombo vya dola ili kubaini uhalali wa mali wanazomiliki.
“Vyombo (vya dola) nataka kuanzia sasa wachunguzeni wafanyakazi ambao walishiriki katika kufanikisha kutorosha almasi zetu, tena wachunguzeni kwa kina,” alisema.
“Angalieni mali zao ikiwa wana mashamba, magari, majumba, viwanja bainisheni.”
Waziri huyo ambaye kila mara alikuwa akirejea neno “Watanzania tumepigwa vya kutosha, nataka Watanzania wajue mali zao”, alisema baadhi ya watumishi kwenye mgodi huo walishirikiana na wajanja wa nje kutoroshea nje rasilimali za Taifa.
“Nasema wachunguzeni na kisha wachukuliwe hatua kuanzia wale waliopo sasa na hata wale waliokuwepo nyuma, lakini kama kuna mtu ametangulia mbele ya haki huyo basi,” alisema.
Akitoa ripoti hiyo, mwenyekiti wa jopo hilo, Profesa Abdulkarim Mruma alisema wamiliki wa mgodi walisema madini hayo yana thamani ya dola 14.8 milioni za Kimarekani.
Lakini baada ya uchambuzi, walibaini yana thamani ya dola 29.7 milioni za Kimarekani, tofauti ya dola 14.7 milioni.
Alisema wamiliki wa mgodi waliweza kufanya udanganyifu huo kutokana na ukosefu wa uzoefu wa watumishi wa Serikali wanaohakiki na kutathmini na baadhi kushirikiana nao.
Alisema walibaini kuwa wamiliki wa mgodi huo huchambua almasi na kuziweka katika makundi tofauti na baadaye huzichanganya wakati wa kuzisafirisha, hali inayochangia udanganyifu wa kiwango na thamani halisi ya madini hayo.
Alishauri Serikali iwe na watu wanaosindikiza almasi hizo hadi Antwep, Ubelgiji ambako husafishwa kabla ya kuingia sokoni, kwa lengo la kujiridha thamani halisi ya soko.
Dk Mpango alisema Serikali imepokea mapendekezo yote na itayafanyia kazi.
“Tunaibiwaje kiasi hiki na sisi tupo,” alisema Dk Mpango mbele ya maofisa wa vikosi vya ulinzi na usalama, uwanja wa ndege na Wizara ya Nishati na Madini.
Alisema kwa udanganyiofu huo, Serikali ingepoteza mrabaha wa dola 882,653.11 na ada ya dola 147,108.85. Maana yake, Serikali ingepoteza jumla ya dola 1,290,761.69, fedha ambazo ni sawa na Sh2.3 trilioni za Tanzania.
Comments