
Hayo yameelezwa Bungeni mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na
Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), alipokuwa akijibu swali la msingi
la Mbunge wa Vwawa Mhe. Japhet Ngailonga Hasunga (CCM), aliyetaka kujua
mikakati ya Serikali katika kuimarisha thamani ya shilingi ya Tanzania
na kupiga marufuku matumizi ya fedha za kigeni nchini.
Akijibu swali hilo Dkt. Kijaji aliainisha kuwa nakisi ya urari wa
biashara, mfumuko wa bei na tofauti ya misimu (seasonal factors) ni
sababu kuu zinazosababisha kushuka na kupanda kwa thamani ya shilingi
nchini.
Dkt. Kijaji aliliambia Bunge kuwa ili kuimarisha thamani ya shilingi
Benki Kuu inaendelea kuthibiti mfumuko wa bei ili usitofautiane sana na
wabia wa biashara nchini.
“Benki Kuu imethibiti biashara ya maoteo (speculation) katika soko la
fedha za kigeni ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa miamala ya fedha za
kigeni inafanywa na benki kwa ajili ya shughuli za kiuchumi tu na sio
biashara ya maoteo, hali hii itasaidia upatikanaji wa fedha za kigeni
katika soko la rejareja ili kupunguza shinikizo la kuporomoka kwa
thamani ya shilingi.”Alisema Dkt Kijaji.
Dkt. Kijaji alifafanua kuwa pamoja na hatua zinazochukuliwa na Benki
Kuu ufumbuzi wa kudumu wa kutengamaa kwa thamani ya shilingi nchini
hutegemea zaidi kupungua kwa nakisi ya urari wa biashara ya bidhaa,
huduma na uhamisho wa mali nchi za nje.
chanzo: zanzibar24.
Comments