IGP Sirro azungumzia tukio la kushambuliwa kwa Tundu Lissu.

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Simon Sirro amewataka wananchi kutoa ushirikiano wa kutosha ili kufanikisha kuwatia mbaroni wahalifu waliohusika kumshambulia kwa risasi Mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lissu.


IGP Sirro ameyasema hayo leo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari na kudai usalama wa nchi upo vizuri na jeshi la polisi limeongeza nguvu ya upelelezi mjini Dodoma ili kuhakikisha linawapata watu ambao wamefanya uhalifu wa kumpiga risasi mbunge Tundu Lissu , huku akiwataka wananchi wasihusishe tukio hilo na masuala ya kisiasa.

“Naomba wananchi wasidanganywe kwenye suala zima la siasa na vitu vingine hapa huwa nasema siku zote kama hakuna amani na usalama siasa haiwezi kupata nafasi ili tukio limetokea tunapeleleza na tupo makini na hili tukio, kwa sasa tumeongeza vikosi vya upelelezi Dodoma, wale waliofanya lile tukio ni lazima tutawakamata ila upelelezi huu unaweza kuzaa matunda mazuri zaidi endapo wananchi watatupa ushirikiano wa kutosha” alisema IGP Sirro.

Aidha IGP Sirro amezungumzia moja ya kauli ya Tundu Lissu aliyowahi kuisema kuwa “kuna watu wananifuatilia” na kuvitaka vyombo vya usalama kuacha kuwatuma watu hao kumfuatilia na kudai kuwa hakuwahi kuripoti katika kituo chochote cha polisi, na kusema sasa usiwe wakati wa kuzungumzia jambo hilo.

IGP Sirro alimalizia kwa kusema kuwa jeshi la polisi lipo imara na lipo kwa ajili ya kulinda watanzania pamoja na mali zao.
chanzo: zanzibar24.

Comments