
Dk. Shein aliyasema hayo leo katika kilele cha
Sherehe za Tamasha la Elimu Bila ya Malipo zilizofanyika katika uwanja
wa Gombani, Wilaya ya Chake Mkoa wa Kusini Pemba na kuhudhuriwa na
viongozi mbali mbali akiwemo Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi
Seif Ali Idd, Spika wa Baraza la Wawakilishi Zubeir Ali Maulid, Mawaziri
na viongozi wengine wa Serikali pamoja na wananchi na wanafunzi kutoka
Unguja na Pemba.
Katika maelezo yake Dk. Shein alisema kuwa kuanzia
Bajeti ya mwaka 2018/2019 Skuli zote za Serikali za Sekondari zitatoa
elimu bila ya malipo ambapo kwa kufanya hivyo ile azma ya Marehemu Mzee
Abeid Amani Karume ya elimu bure itakuwa imekamilishwa.
Aliongeza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inao uwezo huo na
ndani ya Bajeti yake bila ya kumkopa ama kumuazima mtu na hiyo ndio
ahadi yake na ataitangaza rasmi siku itakapoanza kutekelezwa rasmi.
“Hatuna sababu ya kushindwa kutoa elimu bure iwe ya
Maandalizi, Msingi ama Sekondari na naiagiza Wizara ya Elimu na Mafunzo
ya Amali pamoja na Wizara ya Fedha na Mipango wawe makini sana katika
kuipanga Bajeti ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali ya mwaka
2018/2019”,alisema Dk. Shein.
Aidha, Dk. Shein alisema kuwa kwa upande wa elimu
ya Juu utaratibu wa kutoa mikopo utaendelea kama ilivyo hadi pale
zitakapofanywa taratibu nyengine.
Alieleza kuwa ni dhahiri kwamba katika kipindi cha miaka 53 ya
Mapinduzi mafanikio makubwa yamepatikana katika kuyatekeleza malengo ya
Mapinduzi ya Januari 12, 1964 ambapo katika kipindi chote hicho Serikali
imeendelea kutoa elimu bila ya malipo ingawa si kwa kile kiwango cha
miaka 15 ya mwanzo baada ya Mapinduzi.
Alisema kuwa hatua hiyo inatokana na sababu za matatizo ya uchumi na
ongezeko la idadi ya watu yaliokumba nchi ambapo Serikali ililazimika
kuwaomba wananchi wachangie elimu kwa utaratibu maalum ulioandaliwa
kuanzia skuli za Msingi hadi Sekindari.
Hata hivyo alieleza kuwa kuanzia Julai, 2015 suala la uchangiaji wa
elimu katika skuli za Maandalizi na Msingi kwa Unguja na Pemba
limeondoshwa na Serikali inatoa elimu ya Msingi bila ya Malipo kama
ilivyoamuliwa baada ya Mapinduzi.
Dk. Shein alieleza mafanikio yaliopatikana ndani ya miaka 53 katika
sekta ya elimu ikiwa ni pamoja na kujenga taasisi kadhaa, vyuo vya
ufundi, vyuo vya amali na chuo cha elimu mbadala kwa Unguja na Pemba
ambavyo ni vingi kuliko wakati wa ukoloni pamoja na kuwa na vyuo vikuu
vitatu vinavyoendeshwa na Wazanzibari wenyewe pamoja na kuwagharamia
wanafunzi wote kwa kuwapa mikopo nafuu.
Alieleza kuwa fursa za elimu kwa fani mbali mbali zimeongezeka ambazo
hivi sasa zinafundishwa hapa hapa Zanzibar ambapo takriban wataalamu
1800 wa fani mbali mbali wanahitimu kwenye Vyuo Vikuu vya Zanzibar,
mbali na Taasisi nyengine za elimu ya juu.
Aliongeza kuwa Serikali inazitambua changamoto za walimu na
itaendelea kuchukua hatua katika kukabiliana nazo hatua kwa hatua ambapo
vipaumbele vya Serikali kwa hivi sasa ni kuimarisha ubora wa elimu,
miundombinu ya elimu kwa kujenga skuli mpya, kuyakamilisha majengo
yaliojengwa na wananchi, kuzitengeneza skuli za zamani, kuzipatia skuli
vifaa vya maabara, samani na vitabu.
Dk. Shein aliongeza kuwa Serikali inatambua mchango muhimu wa walimu katika kuimarisha maendeleo ya sekta ya elimu
“ nakiri Walimu mnafanya kazi kubwa nzuri, jitihada zinachukuliwa na
Serikali katika kuyaimarisha maslahi ya walimu ili kuwapa ari ya
kutekeleza wajibu wenu wa kuwalea na kuwapa elimu watotio wetu ili wawe
rasilimali bora zaidi ya kuchangia maendeleo ya nchi yetu na kuwa raia
wema na wazalendo”,aliongeza Dk. Shein.
Dk. Shein alitoa pongezi kwa Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali
pamoja na Waziri wa Habari,Utalii, Utamaduni na Michezo pamoja na
watendaji wao wote kwa kufanikisha Sherehe hizo.
Pia, Dk. Shein aliuhimiza uongozi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya
Amali kuongeza jitihada na nguvu maalum katika kufanikisha michezo kwa
kushirikiana na Wizara ya Habari, Utalii, Utamaduni na Michezo.
Mapema Dk. Shein alipokea maandamano ya wanafunzi walioshiriki michezo ya elimu bila ya malipo mwaka huu wa Unguja na Pemba.
Nae Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Riziki Pembe Juma alieleza
kuwa uongozi wa Wizarav yake taendelea kuimarisha sekta ya elimu na
kuhakikisha kuwa juhudi zitaendelea kuchukuliwa katika kuhakisha walimu
wanataoa elimu bora.
Pia, Dk. Shein aliwapongeza washindi na walioshindwa katika michezo
mbali mbali na shughuli za sanaa za mwaka huu na kutoa zawadi kwa
washindi mbali mbali wa michezo pamoja na kushuhudia mashindano ya
michezo yakiwemo mbio za vijiti, mashindano ya watoto wa maandilizi
walioonesha umahiri wao katika mbio za magunia na mbio za miguu mitatu.
Sherehe hizo zilipambwa kwa nyimbo mbali mbali zilizoimbwa na wanafunzi.
chanzo: zanzibar24.
Comments