Ripoti kuhusu uchimbaji na biashara ya madini ya almasi na Tanzanite imeibua jambo jipya. Zaidi ya kuwataja mawaziri wawili wa zamani na wengine wawili wa sasa kuhusika katika dosari zilizosababisha nchi kupoteza fedha nyingi, imefungua mlango mpya wa kuwashughulikia wanasiasa wenye tuhuma za ufisadi.
Spika wa Bunge, Job Ndugai ndiye alikuwa kwanza kueleza kusikitishwa na wanasiasa hao hasa wabunge ambao wamekuwa wakitajwa katika ripoti nyingi za ufisadi,
lakini bado wanarejea bungeni kwa kuchaguliwa na wananchi. Anasema pamoja na wabunge hao kutajwa kwenye matukio ya namna hiyo bado wakirudi majimboni wanachaguliwa na wananchi kwa kuwa wao hawajui tabia zao.
“Vyama vya siasa vinawapitisha, wanashinda ubunge na wakija mimi nitawaapisha na juzi Profesa Lipumba (Ibrahim) kaniletea wapya nimewaapisha,” anaeleza Ndugai.
Kauli hiyo ya Spika Ndugai ndiyo ilimfanya Rais Magufuli kusema ni kweli kuna watu wametajwa kwenye ripoti nyingi na wakiwa bungeni wamekuwa wakichangia hoja kwa nguvu zote.
Rais Magufuli alimuuliza Spika Ndugai kama bungeni wana utaratibu wa kuwashghulikia watu wa namna hiyo au hata kubadili kanuni ili waweze kushughulikiwa. Hata hivyo, alisema kwa kuwa yeye ni mwenyekiti wa CCM anasubiri barua ya Spika na ikiwafikia watashughulikia kwa mujibu wa miiko ya chama chao huku akiamini na vyama vingine vitafanya hivyo.
Huu unaweza kuwa mwanzo wa kuteketeza kichaka cha wanasiasa wenye tuhuma za ufisadi kuwania nafasi za uongozi ndani ya vyama vya siasa, hasa chama tawala.
Hoja ya kuwabana wanasiasa wenye tuhuma za ufisadi ziliibuka baada ya wanasiasa wengi hasa wabunge kutajwa kwenye ripoti mbalimbali za ufisadi.Wabunge wa CCM waliotajwa katika ripoti hiyo na ambao hawana nafasi serikalini kwa sasa ni William Ngeleja, ambaye alitajwa sakata la escrow, makinikia na sasa Tanzanite na Profesa Sospeter Muhongo.
Pia, wakati wa ripoti hizo zikiwasilishwa kwa Spika Ndugai, Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe alishauri zijadiliwe bungeni ili kuja na mapendekezo ya pamoja ambayo yatachukuliwa kama azimio la Bunge, ambalo litatoa maelekezo kwa Serikali ju ya jinsi ya kuzishughulikia.
Hata hivyo, Spika alisema kufanya hivyo itakuwa ni kurudi nyuma, hivyo yeye akaamua kuziwasilisha moja kwa moja serikalini ili zifanyiwe kazi huko huko.
Hatua kwa mawaziri
Kabla ya tukio lililohusisha madini ya almasi na Tanzanite, Rais Magufuli alitengua uteuzi wa Profesa Sospeter Muhongo aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini.
Profesa Muhongo alihusishwa na ripoti ya mchanga wa madini na sasa amebaki na wadhifa wake wa ubunge.
Hata kabla nafasi yake ya uwaziri wa nishati na madini haijajazwa, Profesa Muhongo ambaye pia ni mbunge wa Musoma Vijijini pamoja na mbunge wa Sengerema, Ngeleja wametajwa tena kwenye ripoti za almasi na Tanzanite. Ngeleja aliwahi kuvuliwa uenyekiti wa kamati ya katiba, sheria na utawala ya Bunge baada ya kutajwa pia kwenye ripoti ya Escrow.
Mawaziri wa sasa waliotajwa kwenye ripoti hizo ni George Simbachawene ambaye ni Waziri wa Tamisemi na Edwin Ngonyani (naibu waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano) na wote wamejiuzulu.
Simbachawene aliteuliwa kuwa Waziri wa Madini na Nishati 2015 baada ya Rais wa Serikali ya Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete kufanya mabadiliko katika Baraza la Mawaziri kutokana na kashfa ya uchotwaji fedha kutoka Akaunti ya Tegeta Escrow iliyoondoa mawaziri wawili, akiwamo Profesa Muhongo, ambaye aliwajibishwa kwa kutowajibika vyema kulinda mapato ya Serikali.
Katikati ya ripoti
Akisoma ripoti ya Kamati ya Tanzanite iliyoundwa na wajumbe 11, mwenyekiti wa kamati hiyo, Dotto Biteko anasema imebaini kuwa Tanzania haijawahi kunufaika na madini hayo licha ya kupatikana kipekee nchini. Anasema ni asilimia 20 pekee ya madini hubaki nchini huku asilimia 80 ikiwanufaisha wageni.
Biteko anasema Taifa limeingia hasara kubwa kutokana na ubia uliopo kati ya Shirika la Madini (Stamico) na kampuni ya Tanzanite One (TML) huku baadhi ya watendaji wakihusika kwa kupitisha usajili na mikataba kinyume cha sheria za madini.
Anaongeza kuwa mwaka 2015 Simbachawene akiwa wizarani hapo, aliridhia kuuzwa kwa hisa za kampuni ya Tanzanite One kwa kampuni ya Hong Kong ya Sky Associate Limited ambayo haijasajiliwa na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela) wala kuwa na hati safi za ulipaji kodi na kutofuata ushauri wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Kamishna wa Madini pamoja na Kamati ya Bunge.
Kampuni hiyo ya Tanzanite One iliuza hisa za Dola 22.5 milioni kwa kampuni ya Sky Associate Limited ambayo baadhi ya wamiliki wake ni Watanzania.
Hatua hiyo ilisababisha kampuni ya Tanzanite One kukwepa kodi ya Sh21.85 bilioni ambayo ilikuwa inadaiwa kwa wakati huo na haijalipwa hadi sasa.
Mbali ya Simbachawene, naibu waziri Ngonyani wakati huo akiwa kaimu mkurugenzi mtendaji wa Stamico, alitoa taarifa kwa umma juu ya maridhiano hayo ambayo yamedaiwa kusababisha hasara kwa kulinyima shirika hilo la umma nguvu ya uamuzi kwenye kampuni ya Tanzanite One waliyoingia ubia wa asilimia 50 kila mmoja kuendesha mgodi wa Mererani.
Ripoti hiyo inaeleza kuwa dosari katika utoaji wa leseni, maudhui ya mikataba na utekelezaji mbovu umesababisha hasara ya zaidi ya Sh157 bilioni na upotevu wa tani mbili za tanzanite kwa kipindi cha mwaka 2014 hadi mwaka huu.
Kamati ilieleza kuwa Ngeleja aliyekuwa waziri, aliiacha kampuni hiyo kuendelea kuchimba madini pasipo na leseni kwa kipindi cha miaka mitatu (2010-2013) na kusababisha hasara ya Sh37 bilioni kutokana na ucheleweshwaji wa leseni.
Inasema Profesa Muhongo alitoa leseni hiyo bila kupata ushauri wa bodi na kutoa leseni zaidi ya 700 kwenye eneo la Mererani kinyume na taratibu. Pamoja na tuhuma hizo, hakuna njia yoyote ya kuwawajibisha wabunge wenye tuhuma pale wanapowajibika katika nyadhifa zao serikalini.
Mathalan, alipojizulu uwaziri wa miundombinu, Andrew Chenge kutokana na kashfa ya rada, au Anna Tibaijuka kutokana na Akaunti ya Escrow wote walibaki wabunge.
Maoni ya wachambuzi
Akizungumzia uamuzi huo, Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa anasema hoja ya kutana wabunge wabanwe hadi kwenye nyadhifa zao za kisiasa ni mufilisi kwani kutajwa mara nyingi si hoja ya msingi ya kutaka washughulikiwe.
“Hayo ni matamanio yasiyo na mashiko, ni kweli kutajwa mara nyingi kunaleta shaka, lakini si hoja ya kusema huyu mtu abanwe hata asiwepo bungeni,” anasema.
Msigwa anasema cha msingi ni kuacha vyombo vya sheria vifanye kazi yake na kuthibitisha kwa kutoa ushahidi kwa watuhumiwa hao kuhusika moja kwa moja.
“Kauli nyingine aliyowahi kuitoa mkuu wa nchi ni ile aliyosema kwamba wakati mwingine anatamani kuvunja sheria ili kuokoa rasilimali za nchi. Hii ni hatari sana, huwezi vunja sheria kwa sababu ya jambo moja.”
Msigwa anasema kauli za namna hiyo zinaweza kusababisha viongozi wasio waaminifu kutumia kama kinga ya kufanya maovu na kuamua kubadili sheria zilizopo ili wafanye mambo yao.
Mbunge huyo pia anamshangaa Rais Magufuli kumtetea aliyekuwa mwenyekiti wa kamati ya awali iliyoundwa kuchunguza mchanga wa madini, Profesa Abdulkarim Mruma kwamba hakuhusika na hujuma hizo kama alivyotajwa katika kamati ya almasi. Rais Magufuli wakati akipokea ripoti hiyo alimsafisha mwenyekiti huyo kwamba alifanya hivyo baada kutumwa kukusanya taarifa.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya almasi, Profesa Mruma amethibitika kuhusika moja kwa moja kusaini mikataba ya uuazaji wa madini na kumnukuu alijitetea kwamba alisaini mikataba hiyo bila kuisoma.
Msigwa anaeleza kushangaa Rais Magufuli kudai kuwa alimtuma Profesa Mruma ilihali wakati anasaini mktaba huo yeye hakuwa rais.
“Haiingii akilini leo tunaambiwa eti Mruma alitumwa, hivi wakati anatumwa Magufuli alikuwa Rais kweli. Atueleze alitumwa na nani na wakati huo yeye alikuwa wapi?
Akizungumzia suala hilo, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Ruaha, Profesa Gaudence Mpangala anasema hakumwelewa Rais Magufuli alikuwa anamaanisha nini kuhusu kuwabana wanasiasa.
Anasema kama alitaka kuundwa chombo kwa aajili ya kuwashughulikia wabunge wakati hata ripoti zilizosomwa ni matokeo ya kamati za Bunge, ambazo ndio chombo chenyewe.
Hata hivyo Profesa Mpangala anasema ni vizuri watu wakatambua suala la madini si jipya na kwamba watu walishalalamikia muda mrefu kutokana na kusababishwa na mfumo mbovu.
“Mfumo mbovu ndiyo uliosababisha wahusika hawa kupatikana na hawa wahusika ndiyo walitumia mfumo huo kufanya mambo haya na kutufikisha hapa tulipo,” anasema.
Profesa Mpangala anasema ili kujitoa katika ubadhirifu ni wakati sasa wa Serikali kubadili mfumo mzima kwa kuwa kuwawajibisha watuhumiwa pekee hakusaidii.
Comments