Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani linamshikilia kijana mmoja mkazi wa Kijiji cha Vilabwa, Wilaya ya Kisarawe, kwa tuhuma ya kumchoma kisu na kumuua mwenzake chanzo kikiwa ubishani wa makalio ya mwanamke aliyaepita njiani.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Jonathan Shanna amethibitisha kutokea kwa tukio hilo akieleza kuwa, mtuhumiwa huyo anayejulikana kwa jina la Ramadhani Habibu amekamatwa kwa kosa la kumuua Emmanuel Nassor miaka 26 kwa kumchoma na kisu kifuani baada ya kubishana kuhusu ukubwa wa makalio ya msichana aliyewapita wakipiga soga kijiweni.
“Kuna mdada alipita sasa marehemu na mtuhumiwa walikuwa na wenzao kijiweni wakaanza kuzozana kuwa yule mdada ana chura wengine wakasema la kawaida.”
Kamanda Shanna alisema ubishi ulikuwa mkubwa ndipo Ramadhani kwa hasira akakimbia nyumbani kuchukua kisu alichokitumia kumchoma mwenzake hadi kumuua.
Alisema mtuhumiwa alikimbia ambapo siku ya Septemba 27 majira ya saa 2.30 asubuhi alikamatwa.
Kamanda huyo aliwaasa vijana kuacha tabia ya kupoteza muda vijiweni badala ya kujishughulisha kimaendeleo .
chanzo:zanzibar24.
Comments