Amir wa Makkah, Khalid al Faisal amesema kuwa mahujaji wa Iran ni "ndugu zetu wa kidini" na amewaombea kheri, baraka na amani.
Televisheni ya al Alam imetangaza habari hiyo na kumnukuu Amir huyo wa Makkah akisema mbele ya waandishi wa habari jana Jumamosi kwamba "mahujaji wa Iran ni ndugu zetu wa kidini na tunawakaribisha katika ardhi takatifu za Saudia."
Amir wa Makkah aidha amesema, mahujaji wa Iran mwaka huu hawakukumbwa na tatizo lolote na akaelezea matumaini yake kwamba watamaliza amali zote za Hija kwa salama bila ya usumbufu wowote.
Ikumbukwe kuwa baada ya kutokea maafa ya Mina katika Hija ya miaka miwili iliyopita yaani 2015, Iran ililalamikia sana uzembe uliofanywa na wasimamiaji wa Hija nchini Saudia mwaka huo, suala ambalo lilipelekea kuzidi kuharibika uhusiano wa nchi hizo mbili kiasi kwamba, maafisa wa Saudi Arabia hawakuwaruhusu mahujaji wa Iran kutekeleza ibada ya Hija mwaka jana baada ya nchi mbili kukata uhusiano wao wa kidiplomasia.
Kabla ya kutuma mahujaji wake mwaka huu, Iran ilitaka kupewa hakikisho na viongozi wa Saudia kuhusu usalama wa mahujaji wake na kuepusha kutokea maafa kama ya mwaka 2015, na viongozi wa Riyadh wametoa hakikisho hilo mwaka huu.
chanzo:parstoday.
Comments