Chrispen Kilima, mwenye umri wa miaka 25, amefikishwa mbele ya Mahakama ya Mwanzo akituhumiwa kuiba kompyuta mpakato kwa kujifanya kuwa mwandishi wa redio ya Sauti ya Marekani (VoA).
Akisoma hati ya mashtaka, hakimu wa mahakama hiyo, Edina Sospeter alisema Kilima anatuhumiwa kumtapeli na kumwibia kompyuta mpakato Emmanuel Patrick ambaye ni mtoto wa mwandishi wa habari wa gazeti la Majira, Patrick Mabula.
Alidai kuwa tukio hilo lilitokea ofisi iliyopo eneo la Market Square mjini Kahama baada ya kujifanya mwandishi wa habari wa Voice of Amerika.
Alisema siku hiyo ya Agosti 22, mtuhumiwa alifika ofisi hizo na kujitambulisha kuwa anaitwa Emmanuel Gunze na kwamba ni mwandishi wa habari wa VoA.
Hakimu alisema mtuhumiwa huyo alitaka alimrubuni mtoto huyo kuwa anaazima kompyuta hiyo, lakini alitoweka nayo na kwenda kuiuza wilayani Sengerema mkoani Mwanza kabla ya kunaswa akiwa Chato mkoani Geita ambako alikimbilia.
Baada ya kusomewa mashtaka hayo, mtuhumiwa alikana kufanya makosa hayo na hakimu akaweka wazi dhamana yake, akiweka sharti la mdhamini mmoja kusaini hati ya dhamana ya ya Sh600,000.
Kesi imeahirishwa hadi Septemba 13 itakapotajwa tena kesi hiyo.
chanzo:Mwananchi.
Comments