Acheni jazba mkitoa maoni ya katiba, sheria : ZLSC Pemba.

Wananchi wa Mkoa wa kusini Pemba, wametakiwa kuacha jazba na mzaha wakati wanapoitumia haki yao ya kutoa maoni, juu ya uundwaji wa sheria au katiba, ili kuepusha malalamiko wakati sheria zinapotekelezwa .

Wananchi hao wameelezwa kuwa, katiba na sheria ndio miongozo mikuu ya nchi yoyote ile ulimwenguni, hivyo ikitokezea serikali inapita kukusanya maoni juu ya katiba au sheria, lazima wawe makini na kuacha jazba za kisiasa.

Ushauri huo umetolewa na Afisa Mipango wa Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar ZLSC tawi la Pemba, Khalfan Amour Mohamed, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari, mara baada yakumalizika kwa mikutano ya wazi ya kuwahamasisha wananchi kuisoma katiba, iliofanyika skuli ya Ngwachani na Kituo cha ununuzi wa karafuu ZSTC Tundauwa, Mkoa wa kusini Pemba.
Afisa Mipango huyo alisema, haki ya kutoa maoni ya kwenye katiba au utengenezaji wa sheria, inahitaji utulivu wa hali ya juu kwa wananchi.
Alisema iwapo wananchi watafanya mzaha na kushindwa kuitumia vyema haki yao ya kutoa maoni, wanaweza kujuta wakati sheria zinapotekelezwa.
“Unaweza kusema sheria za nchi hii mbaya, au katiba imetoa mamlaka makubwa kwa taasisi moja, mfano mahakama, kumbe ni kwa sababu tu wakati wa kutoa maoni, watu walifanya kejeli, mzaha na jazba”,alifafanua.
Katika hatua nyengine Afisa Mipango wa ZLSC, Siti Habib Mohamed, alisema hakuna kinga kwa mtu aliefanya kosa na kusingizia alikuwa haelewi sheria.
Hivyo, amewashajihisha wananchi wa mkoa wa kusini Pemba, kufanya kila hila, ili kuzisoma katiba na sheria nyengine mbali mbali za nchi.
“Sisi Kituo cha Huduma za Sheria tunatoa msaada na ushauri wa kisheria bila ya malipo, hivyo njooni muelewa walau haki na wajibu wenu uliomo ndani ya katiba yetu”,alieleza.
Baadhi ya wananchi waliozungumza na mwandishi wa habari hizi kwenye mikutano hiyo, walisema kazi inayofanywa na ZLSC ni nzuri, ingawa inahitajika kila wakati kufanywa.
Moza Idd Makame wa Tundauwa wilaya ya Chakechake, alisema kama watakuwa na utaratibu wa kuwapitia wananchi kila wakati, wanaweza kujua haki na wajibu wao.
Nae Madina Mjaka Himid wa Ngwachani wilaya ya Mkoani, alikishauri Kituo hicho cha Huduma za Sheria Zanzibar ZLSC tawi la Pemba, kuelekeza nguvu zao kwa wanafunzi.
“Sisi huku mitaani tunakuwa na shughuli nyingi, labda waje kama vile karibu na uchaguzi, au wakati wa utoaji wa maoni kwenye katiba, lakini kama watajikita skuli, taifa litakuwa na vijana imara baadae”,alieleza.
Mapema wasanii kutoka Kampuni ya ‘Jufe Film Production’ ya Wete Pemba wakiongozwa na msanii Nguli Mohamed Kombo ‘Mwinyi mpeku’ waliwaburudisha wananchi hao kwa igizo lililovuta hisia, kuonyesha athari kwa wananchi wasioisoma katiba.
Tayari Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar ZLSC tawi la Pemba, kimeshawafikia wananchi zaidi ya 350 wa vijiji vya Konde, Pandani, Tumbe, Ngwachani na Tundauwa kwa ajili ya kuwahamasisha, juu ya kuisoma Katiba ya Zzanzibar ya mwaka 1984.
chanzo:zanzibar24.

Comments