
Akizungumza na Zanzibar24 huko ofisini kwake Vuga, Mkuu huyo wa Mkoa
amesema kuna mambo mengi ambayo Dk. Shein ameagiza yatekelezwe wakati
akifanya tathmini ya ziara yake ya siku mbili mkoani humo.
Alieeleza kuwa wajibu wa kutekeleza maagizo hayo si jambo la hiyari
na kwamba kila mtendaji katika ngazi zote anapaswa kufanya kazi
aliyopangiwa kwa kasi ile ile anayoitaka Mhe. Rais.
“Ni lazima tuhakikishe tunakwenda kwa kasi inayotakiwa na kama kuna mtu asiyeweza kuendana na kasi hiyo ni bora akae pembeni,” alisisitiza Ayoub.
“Sasa ni wakati wa kazi tu uzembe mwiko, na
watakaozembea hatutawafumbia macho wala kuwaonea muhali. Ninafanya hivi
kwa kutekeleza agizo la Mhe. Rais ambao ni wajibu wangu kikazi,” aliweka bayana.
Aidha alisema miongoni mwa changamoto atakazozishughulikia ni
msongamano wa magari katika maeneo ya Mji Mkongwe, uchangiaji damu kwa
hiyari, kutokomeza malaria na kuwakamata watu wanaokaidi marufuku ya
kuingiza wanyama maeneo ya mjini.
Kuhusu tatizo la idadi kubwa ya wanafunzi maskulini, alisema ujenzi wa madarasa uliozinduliwa hivi karibuni kupitia kampeni ya ‘Mimi na Wewe’ unatarajiwa
kupunguza kwa kiasi kikubwa msongamano uliopo kwa sasa baada ya
kukamilika ujenzi huo ambao pia unafanyika katika skuli nyengine ikiwemo
Sharifu Msa.
Alieleza kuwa, wingi wa Wanafunzi katika darasa moja ambapo katika
baadhi ya skuli hufikia 160, haukumfurahisha Mhe. Rais, ambapo
alipongeza juhudi za ujenzi wa madarasa mapya unaofanyika kwa nguvu za
wananchi chini ya uongozi wa mkoa huo.
Baadhi ya miradi iliyotembelewa na Dk. Shein katika ziara yake mkoani
humo, ni ule wa kuhifadhi mazingira katika bahari ya Kilimani ambapo
maji yamekuwa yakipanda hadi katika maeneo ya makaazi ya wananchi.
Aidha alifungua jengo la Chuo cha Utalii Maruhubi, ujenzi wa
barabara ya Kinuni, nyumba za kisasa Fumba na Nyamanzi na mradi wa maji
safi na salama Bumbwisudi pia alifungua skuli ya Kihinani.
Dk. Shein pia alitembelea uwanja wa Mao Tse Tung unaofanywa na wataalamu kutoka Jamhuri ya Watu wa China.
Wakati huohuo, Mkuu wa Mkoa alipokea hundi ya shilingi 15,000,000
kutoka kampuni inayotoa huduma za kiufundi mijini na vijijini (Urban and
Rural Engeneering Service Company) yenye ofisi zake Mikocheni jijini
Dar es Salaam.
Fedha hizo zilizotolewa na Naibu Mkurugenzi wa kampuni hiyo Salum
Mussa Omar, ni kwa ajili ya kusaidia upatikanaji wa madawati kwa skuli
za msingi Mkoa wa Mjini Magharibi.
chanzo:zanzibar24.
Comments