
Afisa Lishe kutoka Kitengo cha Lishe Wizara ya Afya Fatma Ali Said
ameeleza hayo katika ukumbi wa wizara hiyo Mnazimmoja alipokuwa
akizungumza na waandishi wa habari katika maadhimisho ya wiki ya
unyonyeshaji iliyoanza jana.
Alisema maziwa ya mama pekee katika kipindi cha miezi sita ya mwanzo
yanamkinga mtoto na maradhi mengi kwani yanavirutubisho vya kutosha vya
kuwawekea kinga na kujenga upendo baina yake na mama.
Afisa huyo alisema mama anaponyonyesha mtoto kipindi hicho bila
kumpa kitu chengine inapunguza kutoka damu nyingi katika siku 40 baada
ya kujifungua na humsaidia kurudi katika hali yake ya kawaida kwa
haraka.
Alikumbusha kuwa kunyonyesha mtoto maziwa ya kifua pekee katika
miezi sita ya mwanzo hakuna gharama kwa wazazi na baadhi ya akinamama
inawasaidia kujiepusha na mimba nyengine katika kipindi hicho na
kupelekea uzazi wa mpango.
Alisema bado jamii kubwa ya Wazanzibari haina mwamko wa kunyonyesha
maziwa ya mama pekee miezi sita ya mwanzo na utafiti uliofanywa mwaka
jana unaonyesha ni asilimia 20 tu ya akinamama ndio wanaonyonyesha kwa
kutumia utaratibu huo.
Aliongeza kuwa madai ya baadhi ya watu kwamba maziwa ya mama pekee
bila chakula chengine hayamtoshelezi mtoto hayana ukweli iwapo mtoto
atanyonyeshwa kwa muda unaotakiwa.
Alisema mtoto anatakiwa anyonye kwa dakika zisizopungua 20 bila
kupumzika ili apate maziwa yalioko mbali ambayo ndio yenye chakula na
mafuta kwa ajili ya kumjenga mtoto.
“Maziwa ya mwanzo ya mama yanamaji mengi lakini maziwa yanayochelewa
kwa dakika 20 yanavirutubisho vyote muhimu katika makuzi ya mtoto,”
aliongeza Afisa Lishe.
Aliwataka akinamama wanaofanyakazi sehemu mbali mbali kufanya juhudi
ya kuwakamulia maziwa watoto wao na kuyahifadhi vizuri ili waweze
kupewa wakati hawapo majumbani.
Aidha aliwakumbusha akinamama kuendelea kunyonyesha watoto wao iwapo
itatokea bahati ya kupata mimba nyengine wakati mtoto aliezaliwa bado
anaumri mdogo kwani maziwa ya mama mjamzito hayana madhara yoyote kwa
mtoto.
Kilele cha wiki ya unyonyeshaji kitakuwa tarehe 7 mwezi huu katika
Wilaya ya Micheweni na kauli mbiu ya mwaka huu Tudumishe unyonyeshaji
kwa pamoja.
chanzo:Zanzibar24
Comments