Wenye vyeti vya elimu ya darasa la saba waondolewa kazini.

Watumishi wa umma waliodanganya kuwa na vyeti vya kidato cha nne na ambao hawajaviwasilisha kwa waajiri wao, ambao miongoni mwao wana vyeti vya darasa la saba, wameanza kuondolewa katika kazi utumishi wa umma.
 
Tayari baadhi ya taasisi za umma zimeanza kuwaondoa watumishi hao, kutekeleza agizo la Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, inayotaka watumishi  wanaodai kuwa na elimu ya kidato cha nne, lakini hawajawasilisha vyeti pia waliosoma darasa la saba, kuondolewa katika malipo kuanzia mwezi huu.
 
Akizungumza na gazeti la Habarileo jana jioni kwa simu, Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dk Laurean Ndumbaro alikiri kutolewa agizo la kuwaondoa katika mishahara watumishi ambao hawajawasilisha vyeti vyao vya kidato cha nne.
 
“Hao siyo wa darasa la saba, ni waliojifanya wamefika kidato cha nne lakini hadi sasa hawajawasilisha vyeti vyao. Sheria pia ilitaka kuanzia mwaka 2004 watumishi wenye kidato cha nne ndio waajiriwe kwenye utumishi, sasa kama wapo walioingia kwa upendeleo au kwa makusudi, ndio tumeagiza mwisho wa mwezi huu wasitishiwe mishahara yao,” alifafanua Dk Ndumbaro.
 
Dk Ndumbaro alieleza kuwa watumishi hao si wengi, kama wale waliogundulika kughushi vyeti hivyo vya elimu walikuwa 9,932, na imebainika kuwa wafanyakazi 38 kati ya 150 waliokuwa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Mkuu (CDA) waliohamishiwa Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma wameondolewa kazini kwa kuwa na vyeti vya darasa la saba.
 
Aidha, taarifa kutoka ndani ya Shirika la Elimu Kibaha mkoani Pwani zinaeleza kuwa watumishi zaidi ya 100 wameondolewa kutokana na kuwa na elimu ya darasa la saba.
 
“Mwaka 2006 watumishi wengi waliondolewa kwenye mfumo wa ajira ya muda mfupi na kupewa ajira ya kudumu, na kufuatia miradi mingi kufa, wafanyakazi wengi walihamishiwa maeneo mengine hususani hospitalini ambako walitawanywa kwenye vitengo na kufanya kazi pasipokuwa na ujuzi na elimu ya masuala ya afya.
 
“Sasa kutokana na agizo la kuwaondoa wale wenye elimu ya darasa la saba ambao hawajajiendeleza na waliajiriwa kuanzia mwaka 2004, watumishi zaidi ya 100 wamekumbwa na baadhi walikuwa wanakaribia kustaafu,” kinasema chanzo cha habari. Uongozi wa shirika hilo umeahidi kulizungumzia suala hilo leo.
 
Wafanyakazi hao wameondolewa kazini kutokana na waraka wa serikali uliotolewa mwaka 2004, kwamba watumishi wa sekta mbalimbali wajiendeleze kimasomo na wawasilishe vyeti vyao vya kujiendeleza, lakini wao hawakujiendeleza.
chanzo: zanzibar24.

Comments