Wauguzi wa Hospitali ya Mnazi mmoja waaswa kuchakarika kitaaluma.

Wauguzi na Wakunga nchini wamesisitizwa kuongeza bidii katika kuendeleza taaluma katika fani yao  kwa lengo la kutoa huduma kwa ufanisi wakati wa kutekeleza majukumu yao.

Hayo yameelezwa leo huko Hospitali ya Mnazi Mmoja na Mkuu wa Skuli ya Wauguzi na Wakunga wa Chuo Kikuu cha Aga Khan nchini Kenya Profesa Sharon Brownie alipokuwa akizungumza na wasimamizi wa wauguzi  na wakunga wa Hospitali hiyo.

Prof. Sharon amesema wauguzi wana nafasi muhimu kwa jamii hivyo ni vyema kutafuta ujuzi kupitia sehemu nyengine kwa lengo la kukuza fani hiyo.
“Asilimia 90 ya wauguzi duniani ni wanawake, wauguzi mnatakiwa kuangalia mitandao ya wauguzi ambayo inatoa taaluma ya uuguzi  kufanya hivyo mtaweza kubadilika kifanisi katika kazi hii ya uuguzi,” alieleza Profesa Sharon
Alifahamisha kuwa fani ya uuguzi inatakiwa kufanyakazi kwa kujituma na mashirikiano katika utendaji na utoaji huduma na kuweza kuinua afya kwa jamii
Alieleza lengo la ziara hiyo ni kuinua na kuboresha Wauguzi pamoja na Jumuiya za Wauguzi kwa dhamira ya kuendeleza kitaaluma na kutekeleza majukumu ya kazi hiyo kwa ubora pamoja na kuimarisha afya kwa jamii.
Nae Mwenyekiti wa Baraza la Wakunga na Wauguzi Bi Amina Abdulkadir amewataka wasimamizi pamoja na wauguzi kufanya kazi kwa kujiamini, kujiheshimu pamoja na kubadilika kifanisi na kujua majukumu ili kuweza kutekeleza majukumu yao bila ya katawaliwa na kudharauliwa na wengine.
“Muuguzi anatakiwa  kufanya kazi kwa kujiamini, awe smati, ajiheshimu pia anatakiwa kubadilika kielimu sio awe regerege awe ni mwenye kufanya maamuzi  ndio mfanyakazi mwengine nae atamuheshimu, sisi tunataka wauguzi muwe juu zaidi katika fani hii,” alifahamisha Bi Amina.
Aidha Bi Amina amewasisistiza wauguzi hao kuipenda kazi yao kwa lengo la kutoa huduma iliyo bora kwa jamii ili kuepukana na usumbu na malalamiko yanayotolewa na jamii.
Nao wauguzi hao walisema wanafanyakazi katika mazingira magumu hivyo wanahitaji kupatiwa elimu na vifaa vya afya ili waweze kujiimarisha zaidi na kutoa huduma bora kwa jamii.
Aidha wauguzi hao walisisitiza kufanya utafiti katika kazi zao ili kuweza kujua na kupata sababu zinazoikumba jamii wakati wa utoaji huduma kwa lengo la kuimarisha afya na kuepukana na changamoto zinanajitokeza.
chanzo:zanzibar24.

Comments