Raia wa Rwanda leo wanaelekea kwenye masanduku ya kupigia kura kumchagua rais mpya wa nchi hiyo. Watu wanaokadiriwa kuwa milioni 6.8 wanatarajiwa kushiriki katika zoezi hilo ambalo lilianza jana kwa kupiga kura wanyarwanda wanaoishi nje ya nchi.
Vituo 2,340 vimesambazwa kote nchini Rwanda na vilitarajiwa kufunguliwa mapema leo saa moja kamili asubuhi kwa wakati wa Rwanda.
Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Rwanda, Charles Munyaneza amesema anatarajia uchaguzi wa leo utafanyika kwa amani na utulivu kutokana na maandalizi mazuri yaliyofanyika. Munyaneza amesisitiza kuwa, matokeo ya awali ya uchaguzi mkuu wa leo nchini Rwanda yataanza kutolewa leo usiku.
Wagombea watatu wanachuana katika uchaguzi wa leo na inatabiriwa kwamba rais wa sasa wa nchi hiyo Paul Kagame atapata ushindi mkubwa.
Wagombea wengine ni Frank Habineza, wa chama cha Democratic Green Party of Rwanda na Bwana Philippe Mpayimana anayejitegemea.
Waangalizi 2000 kutoka nje ya nchi wanasimamia uchaguzi wa leo nchini Rwanda ambao utagharimu franga bilioni 6.2.
Uchaguzi wa leo nchini Rwanda unafanyika kwa amani japokuwa ofisi ya shirika la Amnesty International katika kanda ya Afrika mashariki imetahadharisha kwamba huwenda ukafanyika katika anga ya hofu inayotokana na ukandamizaji wa miaka mingi wa serikali dhidi ya kambi ya upinzani.
chanzo:parstoday.
Comments