
Walisema kuitisha minada hiyo, huwa ni kikwazo kwao kutokana na
ukosefu wa fedha za kukodia mashamba hayo,
ambapo kama wakiyafanyia
tathmini na kisha kukodisha kwa bei isiokuwa ya mnada, wanaweza
kuyamudu.
Wakizungumza na Zanzibar24 kwa nyakati tofauti, wananchi hao
wanaoyatunza mashamba hayo walisema, lazima kwa serikali iwape
kipaumbele cha pekee kwenye kuyakodi mashamba na sio kupitia minada ya
hadhara kama ilivyo sasa.
Walieleza kuwa, wengi wao wanaoyatunza mashamba hayo, ni wanyonge
kifedha na hutumia fedha nyingi kwa kuyafanyia usafi na wengine kupanda
mikarafuu mipya, hivyo lazima kuwe na fungu la huruma, wakati wa zoezi
la uvunaji unapofika.
Mmoja kati wananchi hao anaelitunza shamba lililokuwa la Suleiman
Riyami lililopo shehia ya Chonga, Kombo Abdalla Kombo, alisema yeye
amepanda mikarafuu mipya 100 kwenye shamba hilo, ambalo amekabidhiwa
zaidi ya miaka 15 sasa.
Kombo, alieleza kuwa pamoja na kupanda mikarafuu hiyo, pia ametumia
shilingi 600,000 kulifanyia usafi shamba hilo lenye mikarafuu mikongwe
isiozidi 80.
“Mimi nimetumia gharama kwanza kulitunza, pia kupanda mengine na
nimeweka watu hapa shamba walilinde, sasa ukiniambia nitoe shilingi
milioni 18.1 ili nilikodi kama mnada ulivyofika ni kunionea”,alifafanua.
Nae Is-mail Haji Chuma wa Mizingani alisema kwa vile mashamba hayo,
serikali ilikaa kwa muda mrefu bila ya kuyafuatilia, lazima wawaangalie
kwa jicho la huruma hasa kufuatia msimu huu kuwa mkubwa.
“Sio vyema sisi tunaoyatunza mashamba haya, kutuunganisha kwenye
minada wa jumla jumla, ingependeza kwanza yakafanyia tathimini na wizara
husika na kisha tukagepewa bei na tukishindwa ikiitishwa
minada”,alishauri.
Kwa upande wake Mmanga Makame Mmanga wa Wete, alisema kinyume chake
cha kuwaweka kwenye minada, inaweza kusababisha manun’guniko kwao na
hatimae mashamba hayo, kukosa washughulikiaji hapoa baadae.
Said Juma Ali akizungumza kwa niaba ya Afisa Mdhamini wizara ya
Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi, alisema taratibu zinataka mashamba
hayo kabla ya kukodishwa kuitishwa mnada wa hadhara na kipaumbele kwa
bei itakayofikiwa, huulizwa anaelitunza shamba na sio vyenginevyo.
Afisa Mdhamini huyo alisema, wanaoyatunza mashamba hayo iwe
wamekubali kuyakodi wenyewe kwenye mnada huo wa hadhara au yamekodiwa na
mtu mwengine, hupewa asilimi 40 ya bei iliofikiwa.
“Bei inayofikiwa kwenye mnada wa hadhara iwe anaelitunza kakubali
yeye kulikodi au mtu mwengine, asilimia yake 40 kama kifuta jasho iko
pale pale, lakini sio kuyakodisha siri siri”,alifafanua.
Wakuu wa wilaya za Mkoani na Chake chake wakizungumza kwa nyakati
tofauti, walisema serikali haifanyi zoezi hilo kwa kumuonea mtu, bali ni
kuhakikisha mali yale haishii kwenye mikono ya wachache.
“Zipo eka tatu tatu ambazo zilitolewa na Rais wa kwanza wa Zanzibar
au zile hati zilizotolewa na Rais Aboud Jumbe Mwinyi, kwa walionazo,
wala zoezi hili haliwagusi, lakini hati nyengine kwenye eka tatu
haziotambuliki”,alisema Mkuu wa wilaya ya Mkoani Hemed Suleiman.
Nae Mkuu wa wilaya ya Chakechake Salama Mbarouk Khatib, alisema
anaamini zoezi hilo, linaweza kuyaibua mashamba kadhaa ya serikali,
yaliokuwa mikononi mwa wananchi kinyume na sheria.

chanzo: zanzibar24.
Comments