Wanafunzi wapata ufadhili kwenda kusoma Japan.

Mwakilishi wa Jica Tanzania, Toshio Nagase
Wanafunzi wanane wa Tanzania Bara na Zanzibar wamepata nafasi ya kusoma shahada ya uzamili kwenye vyuo vikuu mbalimbali vya Japan.
Wanafunzi hao wamepata nafasi hiyo baada ya kupita katika usaili uliojumuisha wanafunzi 40 waliojitokeza kuwania nafasi hizo kupitia Mpango wa Kufundishwa Masomo ya Biashara Afrika kwa Vijana Kitaalamu au ABE-Intiative’.

Mpango  huo kwa sasa upo katika awamu ya nne tangu kuanzishwa kwake na unafadhiliwa Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japan (Jica).
Mwakilishi wa Jica Tanzania, Toshio Nagase amesema wanafunzi hao kutoka Zanzibar na Tanzania Bara wanatarajia kuondoka mwisho mwa mwezi huu na mwanzoni mwa mwezi ujao baada ya taratibu zao kukamilika.
Amesema ili kupata nafasi mwombaji anatakiwa awe na vigezo mbalimbali vikiwemo kuongea, kuwasiliana vyema kwa lugha ya kiingereza, awe na afya njema na awe mwanafunzi mwenye shahada inayoendana na programu yao.
“Tangu programu hii imeanza zaidi ya wanafunzi 70 wamenufaika na mpango huu. Kwa miaka mingi nchi yao imewapeleka Japan vijana wenye uwezo kwenda kusoma shahada ya uzamili,” alisema Nagase.
Nagase amewataka wanafunzi waliopata nafasi hiyo kusoma kwa bidii na kwamba wakirudi wataisaidia Tanzania katika kujenga uhusiano imara wa kibiashara na Japan.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora) Dk Lauren Ndumbaro amewataka wanafunzi hao kuwa mabalozi wazuri wa Tanzania pindi watakapokuwa Japan.
“Tumieni nafasi hii kusoma kwa bidii. Pia kuweni mabalozi wa kutangaza vivutio vilivyopo Tanzania ili kuwavutia watalii wa Japan,” amesema Dk Ndumbaro.
Mbali na hilo, Dk Ndumbaro amewataka wanafunzi hao pia kuwa makini katika masomo yao na watumie ujuzi watakaoupata kuisadia Tanzania.
Wanafunzi waliopata nafasi hizo ni John Lukas, Grace Chaula, Kassim Yusuph Hassan, Elizabeth Akaro, Zawadi Macha, Hossen Iddi, Jalali Dakhala Ameir na Haji Rehani Omary.
chanzo:Mwananchi.

Comments