Viongozi walia na uharibifu wa mazingira ya bahari Pemba.

Uokotaji wa Kaure kwa kasi baharini ni moja miongoni mwa sababu inayochangia uharibifu wa mazingira ya bahari na kupelekea athari nyingi kwa viumbe hai waishio katika mazingira hayo.
Hayo yameelezwa na Afisa wa doria Pemba, Khalfan Amour  Juma, wakati alipokuwa akizugumza na waandishi wa habari  katika Ofisi ya wizara ya kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi, Pemba.

Afisa huyo aliendelea kueleza kuwa, kaure ni jamii ya viumbe vyenye kustawisha mazingira ya bahari na kutoa hamasa kwa viumbe wengine kuweza kuishi kwa kutegemea viumbe hivyo.
‘’Kaure zinapokuwa baharini zinapunguza mmongonyoko wa bahari, na ukali wa mawimbi pamoja na kutoa rutuba ya ardhi ya bahari, kama hazitakuwepo viumbe vyengine pia wanaweza kutoweka’’, Khalfan alieleza.
Sambamba na hayo Afisa huyo alisema kuwa, Serikali imekataza uokotaji wa viumbe kaure kutokana na kuibuka kwa wimbi kubwa la wafanyabiashara wa kaure kusafirisha nje ya Zanzibar na kupelekea uharibifu wa mazingira ya bahari.
Alisema kwa sasa, jamii inatakiwa kuwa makini na kuacha kuokota viumbe kaure, ili kurejesha uhalisia na haiba ya viumbe wengine wanaoishi baharini kwa kutegemea viumbe hivyo.
Hata hivyo alisema kuwa, jukumu la utoaji wa elimu ni la Idara ya Uvuvi ambapo imeshaanza kueleza faida na athari za kupotea kwa viumbe hivyo katika mazingira ya bahari, ingawa wako wanaokaidi maelekezo hayo.
‘’Sisi kama idara ni kazi yetu kuelimisha na kupiga marufuku kwa kueleza athari kwanza ndio sheria inafuata, hatuwezi kutekeleza sheria bila kueleza matatizo ya jambo tunalotaka lisifanyike’’,alisema Afisa huyo .
Nae Ofisa Mdhamin, Wizara ya Kilimo Pemba, Sihaba Haji  Vuai, amesisitiza kwa wananchi kufuata taratibu zilizowekwa katika uvunaji wa rasilimali ya Kaure katika bahari, ili kuepusha athari zinazoweza kujitokeza.
Ofisa Mdhamin, alisema kuwa, matumizi ya rasilimali hiyo kwa wanajamii inatakiwa ifanyike kwa kiasi kidogo, ili kueka usawa wa ikolojia kwa viumbe wanaoishi baharini.
‘’Tunapopiga marufuku ya kusafirisha rasilimali hiyo au kuvuna kwa kiasi fulani, tunataka kueka usawa wa ikolojia katika maeneo tofauti, wanajamii wanapofanya ujanja kuondoa hizo kaure athari zitatokezea’’, Sihaba alieleza.
‘’Kuepo kwa kaure katika mazingira ya baharini ni muhimu sana, kuepo kwao kunapunguza uepo wa majani mengi, hivyo viumbe ambao hawapendi kuishi katika majani mengi wanapata kustawi, wananchi wachukue kwa kiasi,kwani zinapokuwa nyingi sana zinaweza kuathiri sehemu nyengine na usawa utakuwa haupo’’, aliendelea kueleza.
Aidha, alisema kuwa, rasilimali ya kaure ambayo inaishi kwa kutegemea majani ya bahari ambapo, kuna viumbe ambao hawawezi kuishi katika majani mengi inaweza kusababisha kutoeka kwa viumbe hao.
Maeneo yaliojitokeza wimbi kubwa la wafanya biashara ya kaure ni Mkumbuu kwa Wilaya ya Chake Chake, Kisiwa Panza, Kangani kwa Wilaya ya Mkoani, na  Makangale, Msuka kwa Wilaya ya Micheweni.

Comments