
Rai hiyo ameitoa wakati akizindua Tawi la CCM la Kitope ‘B’ jimbo
la Mahonda kwenye ziara yake ya kukagua na kuzindua miradi mbali mbali
ya maendeleo aliyoianza leo Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Dkt. Shein alisema viongozi na wanachama wa chama hicho wanatakiwa
kutumia vyema ofisi za Tawi hilo ambalo ni la kisasa kwa lengo la
kutekeleza kwa ufanisi kazi za kisasa zitakazozaa matunda ya ushindi
katika uchaguzi wa mwaka 2020.
“Kwanza nakupongezeni viongozi na wanachama wote wa jimbo la Mahonda
mlioshiriki kujenga tawi hili la kisasa linaloendana na hadhi ya chama
chetu kimaendeleo kwani lina ofisi zote ambazo ngazi zote kiutendaji
ndani ya tawi mtafanya kazi zenu kwa utulivu.
Pia nasaha zangu kwenu ni kwamba uchaguzi mkuu unakaribia haupo mbali
hivyo tumieni ofisi hii vizuri kuchapa kazi kwa bidii sambamba na
kuongeza wanachama wapya ambao ndio mtaji wetu mkubwa wa kisiasa ili
kuhakikisha 2020 tunashinda.”, alisisitiza Dkt. Shein.
Aidha alisema kuwa lengo la serikali ya mapinduzi ya Zanzibar
inayotokana na CCM ni kuimarisha huduma zote za kijamii na kiuchumi ili
wananchi wa mijini na vijijini waweze kunufaika na fursa hizo.
Dkt.Shein ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi alitembelea ujenzi wa kituo kipya cha mashine za kutibia maji
kinachojengwa katika eneo la Donge mbiji ambapo mradi huo uliofadhiliwa
na serikali ya China utagharimu zaidi ya Dola za kimarekani milioni 5.5.
Katika ziara hiyo Dkt. Shein alitembelea shamba la karafuu na
kuzungumza na mliki wa mradi wa kilimo cha karafuu huko Donge Pwani,
Haroun Abou Mbarouk alieleza kuwa shamba hilo lenye mikarafuu zaidi ya
170 limekuwa likizalisha zao hilo kwa wingi ambapo kwa mavuno ya mwaka
wanapata zaidi ya gunia 25.
Sambamba na hayo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi alitembelea mradi wa ujenzi wa tangi la Maji huko Donge
Kisongo unaojengwa na mafundi kutoka jamhuri ya watu wa China
utakaowanufaisha wananchi wa Wilaya ya Kaskazini “B” na maeneo
jirani.
Ziara hiyo itaendelea kesho katika Wilaya ya Kaskazini ‘’A” Unguja
ambapo Dkt.Shein ataweka mawe ya msingi katika miradi mbali mbali ya
kijamii na kuhitimisha kwa hotuba ya majumuisho ndani ya Mkoa huo.
![]() |
![]() |
![]() |
chanzo:zanzibar24.
Comments