Idara
ya Uhamiaji nchini imewataka wananchi kutambua kuwa paspoti siyo
kitambulisho ndani ya nchi na kwamba kisitumike kwa matumizi hayo kwa
sababu siyo utaratibu uliopangwa kisheria ndani ya mipaka ya nchi.
Hayo
yalisemwa jana jijini Dar es Salaam na Kamishna wa Uhamiaji- Pasi na
Uraia, Gerald Kihinga ambapo pia aliwaomba wananchi kutambua kuwa
paspoti zinazotolewa zinapaswa kutunzwa na kutumika kwa lengo
lililokusudiwa la kusafiria nje ya nchi.
Kihinga
alisema kumekuwa na maombi ya kutengenezewa paspoti baada ya kupotezwa,
lakini wengi wamekuwa wakitoa sababu ambazo zinatilia shaka umakini wa
mtu kwenye utunzaji wake.
“Naomba
mfahamu kuwa paspoti pia zinazotolewa siyo vitambulisho ndani ya nchi
hivyo visitumike kama vitambulisho na tena si vizuri kutembea nayo kila
mahali kama huna safari ya nje ya nchi.
"Paspoti
au hati ya kusafiria zinatumika kama kitambulisho pale unapokuwa nje ya
nchi, lakini matumizi yake rasmi ni ya kukusaidia kuingia na kutoka
nchini,” alisema.
Alisisitiza
kuwa kitambulisho rasmi cha Mtanzania anachotakiwa kutembea nacho ni
kile kinachotolewa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA).
Aidha,
kamishna huyo pia ametaka wananchi raia wa Tanzania kutambua kuwa
wanaweza kupata paspoti wakiwa popote Tanzania na kwa muda mfupi.
chanzo:Mpekuziblog.
Comments